23Mei2013

 

Halmashauri yaagizwa kuanzisha miradi ya uvuvi

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuwaanzishia wananchi miradi ya uvuvi wa kisasa wa kutumia mitumbwi mikubwa inayokwenda mbali ili kuinua kipato chao.

Akihutubia mkutano wa hadhara juzi, kuhitimisha ziara yake ya siku moja ya wilaya hiyo, alisema njia nyingine ya kuinua kipato ni kuendeleza kilimo cha kisasa cha mboga, matunda na viungo.

“Wastani wa kipato cha mwananchi wa Ukerewe cha Sh 340,000 kwa mwaka au Sh 960 kwa siku hakifai kumuondolea umasikini. Halmashauri lazima iwaanzishie wananchi miradi ya uvuvi na kilimo cha mboga, matunda na viungo,” alisema.

Aliwataka watendaji na watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo kukaa na kubuni mpango mkakati wa kiuchumi wa wilaya utakaoenda sawia na ule wa kimkoa ili kuona ni namna gani wanaweza kupandisha kipato cha mwananchi.

Aliwataka wataalamu hao kutafuta namna bora ya kuutumia uvuvi ili mazao yake yaweze kumnufaisha mwananchi wa Ukerewe ili aweze kuondokana na umasikini, badala ya mazao hayo kuwanufaisha watu wa kutoka maeneo mengine.

“Katika hili la kutumia samaki na mazao yake, hebu fanyeni kila mnachoweza ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Ukerewe wananufaika na mazao ya samaki ili waweze kuinua hali zao za maisha”, aliongeza.

Aliitaka halmashauri hiyo kuweka mfumo utakaowezesha watu wanaovuna mazao ya samaki kutozwa ushuru ili kurudisha fedha inayotokana na mazao hayo kwa lengo la kuinua hali za vipato vya wananchi na uboreshaji wa makazi ya watu.

Aliendelea kuwaambia viongozi, “Taarifa yenu inaonesha kuwa hamna utaratibu wa kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na mazao ya samaki, kwa wale wanaokuja kununua muwatozeni ushuru ili fedha hizo zirudi kwa wananchi kufanya shughuli za maendeleo”.

Aliwataka viongozi kutafuta namna ya kutumia rasilimali ya maji ya Ziwa Victoria katika kumkomboa mwananchi kiuchumi na kuvutia utalii katika wilaya hiyo yenye jumla ya visiwa 37, ambavyo kati yake, visiwa 15 vinatumika kwa makazi ya kudumu na vilivyosalia vinatumika kwa makazi ya muda mfupi na shughuli za uvuvi.

Ukerewe ni miongoni mwa wilaya saba za Mkoa wa Mwanza na ina ukubwa wa kilometa za mraba 6,400, ambazo kati yake asilimia 90 ni eneo la maji na asilimia 10 ndiyo nchi kavu.

Ni kisiwa kikubwa katika Ziwa Victoria chenye idadi ya watu 260,000. Wastani wa kitaifa wa pato la mwananchi ni zaidi ya Sh 800,000 kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana.

Wastani wa Mkoa wa Mwanza ni Sh 900,000 na kuufanya mkoa kushika nafasi ya saba kwa viwango vya kipato cha mwananchi. Kiwango kinachotajwa kimataifa ni wastani wa Sh 1,500 kwa siku.

Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la nyumba za watumishi wa Serikali Kuu, jengo la maabara ya kisasa kwenye hospitali ya wilaya na alitembelea banda la mfano la mradi wa ufugaji nyuki.