Wakulima waomba Magufuli kufuta ushuru wa mazao

WAKULIMA wadogo nchini wamesema halmashauri nyingi hazirejeshi asilimia 20 ya fedha za tozo za ushuru wanazokatwa katika vijiji kwa shughuli za kimaendeleo ya wananchi, ikiwemo kuboresha mifumo ya barabara kama ilivyokusudiwa na serikali.

Kutokana na tabia hiyo wamemuomba Rais John Magufuli kuwafutia ushuru wa mazao kutokana na wanaonufaika ni watumishi wa halmashauri husika na madiwani kwa ajili ya kujipatia posho badala ya kusaidia shughuli za kilimo .

Wakulima walitoa ombi hilo juzi mjini hapa wakati wa kongamano la kujadili changamoto zinazohusu tozo katika mazao ya kilimo lililoshirikisha wakulima wadogo, maofisa wa biashara na kilimo wa halmashauri pamoja na viongozi wa kisiasa wakiwemo madiwani.

Kongamano hilo limeandaliwa na Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayofanya kazi na wakulima wadogo Tanzania katika kuendeleza usimamizi shirikishi wa matumizi ardhi yanayozingatia Ikolojia (PELUM).

Wakichangia mada hiyo kwa nyakati tofauti baadhi ya wakulima hao walisema kuwa mpaka sasa hawajaona manufaa yoyote ya tozo wanazokatwa wakati wa kuuza mazao yao. Walidai kuwa kinyume chake baadhi ya halmashauri zimekuwa ikizitumia mapato yatokanayo na tozo kwa ajili shughuli mbalimbali ikiwemo vikao vya madiwani na watumishi.

Mmoja wa wakulima wa vitunguu, Abel Rubeini alimuomba Rais Magufuli awafutie ushuru huo wakulima wadogo na ushuru huo utozwe kwa wafanyabiashara wanaokwenda kununua mazao.

Mkulima wa wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Agustino Luanda alimuomba Rais Magufuli kuangalia mfumo mpya wa kuwatoza wakulima wadogo kulingana na mazao wanayozalisha kwa vile tozo hizo zimekuwa zikiwadidimiza kiuzalishaji.

Alipendekeza wakulima wadogo kutozwa asilimia tatu ya mazao yanayozalishwa na kiwango hicho kitumike nchi nzima na si kila halmashauri kujipangia viango vyake ushuru.