Dk Shein ahimiza uadilifu kwa wakusanya kodi
- Imeandikwa tarehe 14 Septemba 2012
- By Mwandishi Maalumu, Zanzibar
- Imesomwa mara: 249
WAFANYAKAZI wa taasisi zinazohusika na ukusanyaji, ukaguzi na udhibiti wa mapato ya Serikali, wametakiwa kuongeza juhudi na kuwa waadilifu katika kuitumikia nchi.
Aidha Serikali imeahidi kuiunga mkono Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili ifanye kazi zake kwa ufanisi zaidi.
Mwito huo ulitolewa jana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, katika hotuba yake ya uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT) lililopo Maisara mjini Unguja.
Aidha, Dk Shein aliwahimiza wafanyakazi wa Serikali waliokabidhiwa dhamana ya kupanga na kutumia fedha za Serikali, kutekeleza wajibu wao kwa kufuata taratibu za kisheria katika kuwatumikia wananchi.
Alisisitiza kuwa jitihada za Serikali na za wananchi hazitoweza kuleta matunda mazuri ikiwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu na Serikali kwa jumla haitekelezi majukumu yake ipasavyo.
“Jengo hili ni ithibati ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha utawala bora na demokrasia.
Pia, ni utekelezaji wa ahadi niliyoitoa wakati nilipokuwa nafungua Baraza la Nane la Wawakilishi tarehe 9 mwezi Novemba mwaka 2010,” alisema Dk Shein.
Hivyo Dk Shein alisisitiza kuwa ufunguzi wa jengo hilo lenye vitendea kazi vya kisasa ni jumla ya mipango madhubuti ya Serikali katika utekelezaji wa ahadi hiyo ambapo gharama zote za jengo pamoja na vifaa vyake vimegharimiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mapema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Fatma Mohammed Said alisema Ofisi hiyo baada ya kukamilisha utekelezaji wa Mpango Mkakati uliopita wa mwaka 2007-2011, imeandaa Mpango Mkakati mwingine wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2011 ambao kwa sasa ndio unaofanyiwa kazi.
Alisema mpango huo ni mwendelezo wa hatua zilizofikiwa katika kuimarisha shughuli za ukaguzi wa hesabu ili uende sambamba na mabadiliko ya ukaguzi na teknolojia duniani kwa kufuata viwango vya ukaguzi kitaifa na kimataifa.



