19Mei2013

 

Soko huru kunufaisha wakazi wa EAC

KUWEPO kwa soko huru kutawanufaisha wafanyabiashara nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo kukuza uchumi wa nchi hizo.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inahusisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Hayo yalisemwa na Rais Jakaya Kikwete katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara nchini Kenya (KAM) jijini hapa juzi.

Rais Kikwete alisema baada ya kukamilisha suala la soko la pamoja, nchi wanachama zinashughulikia kuanzishwa kwa sarafu moja, hivyo kuwataka wafanyabiashara kuandaa mazingira ambayo yatazinufaisha nchi hizo.

Aidha, alisema Tanzania ina nafasi kubwa za uwekezaji na kuwataka wafanyabiashara wa Kenya kuwekeza katika maeneo mbalimbali.

Naye Waziri wa Uchukuzi, Amos Kimunya aliyemwakilisha Waziri wa Biashara, Moses Wetang'ula alisema Tanzania na Kenya zina historia ya muda mrefu ya kuwa na uhusiano mwema hivyo akawataka wafanyabiashara kufanya kazi kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto zilizopo.

Akimkaribisha Rais Kikwete katika hafla hiyo, Makamu Mwenyekiti wa KAM, Pradeep Paunrana alisema kuwepo kwa amani na usalama nchini Tanzania kunawapa nafasi kubwa wafanyabiashara kupeleka miradi yao nchini Tanzania, kwa kuwa wana uhakika na amani iliyopo.

Rais Kikwete ambaye alikuwa nchini hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu alitembelea pia Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) ambacho alisema kinatoa wataalamu walioiva katika mafunzo ya kijeshi na kuongeza kuwa baadhi ya maofisa waliopitia chuo hicho kutoka Tanzania walionesha kuridhishwa na mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.

Alisema Tanzania ambayo imeanzisha chuo kama hicho eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam ina mambo mengi ya kujifunza kutoka katika chuo hicho ambacho alisema ni cha aina yake katika Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.