20Mei2013

 

SCF kufunda wajasiriamali 100

MFUKO wa Kukuza Ushindani kwa Wajasiriamali Wadogo na Wakati (SCF) umedhamiria kutoa mafunzo kwa wajasiliamali zaidi 100 juu ya usindikaji wa chakula na kuwajengea uwezo wa kushindana kibiashara katika soko la ndani na la kimataifa.

Mkurugenzi wa SCF, Casmir Makoye alisema mfuko huo utahakikisha kuwa unaongeza kasi ya kutoa mafunzo ya kipekee kwa wajasiriamali wadogo na wakati wanaosindika bidhaa za vyakula nchini ili kujenga uwezo wao wa uzalishaji wa bidhaa bora na kuongeza faida yao.

Alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya awamu ya tatu yatakayochukua wiki moja mjini hapa yakiwahusisha wakurugenzi watendaji na wafanyakazi wa kampuni zinazosindika vyakula nchini.

Makoye alisema kuwa taasisi yake imepanga kufanya mafunzo mengine mwezi ujao ikijikita katika usindikaji wa maziwa.

Wafanyabiashara wadogo na wa kati watafundishwa jinsi ya kuzalisha bidhaa za ziada mbali na kuendelea a uzalishaji uliozoeleka jibini, mtindi na siagi. Pia watapata fursa ya kufundishwa jinsi ya kuongeza vionjo zaidi katika bidhaa zao.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine -Idara ya Kilimo cha Uchumi na Biashara ya Kilimo (SUA - DAEA) chini ya mwamvuli wa Tume ya Ushauri wa Kilimo ya chuo hicho (SUA BACAS) ambayo itaelimisha kuhusu elimu ya uongozi katika biashara.

Mkuu wa SUA – DAEA, Dk Damas Philips alisema kuwa mafunzo yatasaidia wafanyabiashara kuongeza uwezo katika uongozi ndani ya kampuni zao, kuboresha njia za usambazaji wa bidhaa zao na kuwapatia njia bora za jinsi ya kuhifadhi vyakula kwa kufuata viwango vya ndani na vya kimataifa.