Watatu wauawa mapigano ya kugombea mipaka

WATU watatu wa Kijiji cha Kisangiro, Kata ya Kirangi wa kabila la Wasonjo wilayani Ngorongoro Mkoa wa Arusha wameuawa huku mwanamke akijeruhiwa baada ya kuvamiwa na kikundi cha watu wanaosadikiwa kuwa ni Wamasai kutokana na kugombea mipaka ya kijiji.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi na katika mgogoro huo, Wamasai walitumia makasha zaidi ya 20 ya risasi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Mathew Shiloma alikiri kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia juzi ikiwa ni baada ya Wamasai kutoka Kijiji cha Naan, Kata ya Saitosambu kuvamia wakiwa na risasi.

Alisema kabla ya Wamasai hao kuvamia, ilielezwa kuwa wananchi wa Kisangiro walianza kuvamia maboma yao na kujeruhi mwanamke mmoja usiku, hivyo kundi hilo liliamua kulipiza kisasi kwa kuwavamia na kusababisha mauaji hayo.

Alisema mgogoro wa mipaka ya ardhi katika eneo hilo ni wa muda mrefu na Baraza la Madiwani liliamua kuunda Tume kwa ajili ya kushughulikia tatizo hilo ili kuwe na suluhu ya kudumu.