Arusha yapanga kutumia bil 295.1/-

MKOA wa Arusha umepanga kutumia Sh bilioni 295.1 katika matumizi mbalimbali ya miradi ya maendeleo, mishahara na matumizi mengine katika mwaka wa fedha 2016/17. Bajeti hiyo ni ongezeko la Sh bilioni 61.3 sawa na asilimia 26 ikilinganishwa na ya mwaka 2015/16 ambayo ilikuwa Sh bilioni 233.8.

Hayo yamo katika taarifa ya Mkoa iliyosomwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa. Kikao hicho kilihudhuriwa na wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Arusha na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya zote na jiji la Arusha, wabunge na wenyeviti wa vyama mbalimbali vya siasa.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa sehemu kubwa ya fedha za ruzuku ya bajeti ya mwaka 2016/17 zimeelekezwa kwenye kulipa mishahara ya watumishi wa umma asilimia 78, miradi ya maendeleo asilimia tisa na matumizi mengineyo asilimia 13.

Hata hivyo wastani wa asilimia 60 ya mapato ya ndani ya halmashauri za wilaya na Jiji la Arusha yameelekezwa kwenye kugharimia miradi ya maendeleo kwa kila halmashauri husika.

Ntibenda alisema makisio ya mapato ya ndani kwa wilaya saba za mkoa wa Arusha ni Sh bilioni 33.6 na fedha za miradi ya maendeleo zilizotengwa kwa halmashauri hizo ni zaidi ya Sh bilioni 20. Mkuu huyo alisema vipaumbele vya mkoa wa Arusha mwaka 2016/17 ni pamoja na ukusanyaji wa mapato ya Serikali Kuu na ujenzi wa miundombinu ya elimu ya msingi na sekondari.

Miundombinu hiyo ni madarasa, madawati, meza na viti, nyumba za walimu, mabweni, maabara na maktaba. Alitaja vipaumbele vingine ni pamoja na matundu ya vyoo, majengo ya utawala na ununuzi wa vitendea kazi vya kufundishia na kujifunzia katika halmashauri zote saba. Akizungumzia elimu, Mkuu huyo alisema kati ya wanafunzi 27,005 waliofaulu, walioripoti shuleni ni 23,674 ; sawa na asilimia 85.9 .