21Mei2013

 

Wauza samaki Feri wamtaka Waziri wa Uvuvi

UMOJA wa Wakusanyaji na Wauzaji Samaki katika Soko la Feri (Uwasau), umesema hautakubali kulipa ushuru wa nyongeza ya asilimia tano hadi pale mgogoro wao utakapopatiwa muafaka na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kiongozi wa Uwasau, Abeid Seleman, alisema hadi sasa hakuna utaratibu wa kisheria unaoeleweka, unaotumiwa na viongozi wa soko hilo.

Alisema wanamtaka Waziri wa Uvuvi afike haraka kwenye soko hilo.

“Kinachoonekana hapa tumegeuzwa kuwa mtaji na baadhi ya watendaji wa soko hili kwa kutulazimisha kulipa ushuru, hatua hii inashangaza kwa kuwa wakati mwingine wanatuambia kuwa hatuko kisheria katika hili eneo, iweje leo watuambie tulipe ushuru huo,” alisema Seleman.

Alisema wanashangazwa kusikia kuwa uwepo wao pale, hauko kisheria tangu Oktoba mwaka jana, huku baadhi ya watendaji wanaendelea kuwatoza ushuru na wakati mwingine hawapewi stakabadhi.

Seleman alisema hawapingi mipango ya Serikali ya kusimamia vyanzo vyake vya mapato, bali wanapinga ubabe wanaofanyiwa na watendaji hao, kwa kulazimishwa kulipa ushuru huku wakinyimwa baadhi ya huduma katika eneo wanalofanyia kazi.

Alipotafutwa Katibu wa Soko hilo, Mbaraka Kilima alisema suala linalowakabili wafanyabiashara hao ni la kisheria zaidi, ambako sheria imefafanua vizuri kuwa eneo wanalofanyia biashara si rasmi.

Alisema wafanyabiashara hao hawana ujanja, bali wanachotakiwa ni kutii sheria kama inavyowaelekeza kuuza samaki wao katika eneo la mnada, ambalo limetengwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za uendeshaji wa soko hilo.