20Mei2013

 

Benki Afrika Tanzania kuendelea kusaidia wafanyabiashara

BENKI ya Afrika Tanzania imesema itaendelea kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati ili kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi hapa nchini.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa benki hiyo, Ammish Owusu- Amoah aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam kuwa tayari benki hiyo inazo na itaendelea kuvumbua huduma zinazolenga kuwasaidia kifedha wajasiriamali wa hapa nchini.

“Huduma zetu zinalenga kutoa suluhisho la kifedha ili kuendeleza kada hii muhimu kwa maendeleo,” alisema.

Kwa mujibu wa Ammish, uwezo wa chombo hicho cha fedha kutoa mikopo ulikua kwa asilimia 31 mwaka jana na kuwa fedha nyingi zilienda kwa wajasiriamali.

Alisema mtandao wa benki hiyo nchini katika maeneo kama Tunduma, Mbeya, Moshi, Arusha, Mwanza, Morogoro, Kahama na Mtibwa kwa kiwango kikubwa unalenga kusaidia wajasiriamali katika maeneo hayo.

Alisema benki hiyo inatoa huduma kwa wasafirishaji, wasambazaji, hoteli na biashara nyingine za wajasiriamali hapa nchini.

Alisema pamoja na huduma hizo za kifedha kwa wafanyabiashara, benki hiyo inaelewa changamoto zinazowakabili na hivyo inajitahidi kuja na huduma maalumu ambazo zinalenga kuwasaidia kuendelea na shughuli na kuongeza uzalishaji.

Alisema pamoja na hali ngumu ya kiuchumi na mfumuko wa bei, iliyoshuhudiwa katika mataifa mbalimbali mwaka jana, bado benki hiyo iliweza kuongeza idadi ya watu wanaoweka fedha kwa asilimia 17 na kufikia bilioni 264.

“Hii ilisababishwa na timu imara ya mauzo tuliyonayo,” alisema na kuongeza kwamba kwa ujumla faida kabla ya kodi kwa mwaka 2012 iliongezeka mara mbili (ongezeko la asilimia 101 kulinganisha na mwaka uliotangulia) na kufikia Sh bilioni 3.3.

Hadi sasa ina matawi kumi jijini Dar es Salaam pamoja na mengine nane katika maeneo ya Morogoro, Tunduma, Mwanza, Moshi, Mbeya, Mtibwa, Arusha na wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga.

Benki hii ni moja ya mtandao wa kibenki unaofanya kazi katika nchi 15 ambazo ni Benin, Burkina Faso, Ghana, Ivory Coast, Mali, Niger, Senegal, Burundi, Djibouti, Kenya, Madagascar, Tanzania na Uganda. Pia ina tawi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).