Watakiwa kusimamia ugawaji fedha za vikundi

WIZARA ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya nchini kuhakikisha wanasimamia ipasavyo utolewaji fedha zinazotengwa kwa ajili ya vikundi vya akinamama na vijana bila urasimu.

Naibu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jaffo, alitoa agizo hilo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Tweve (CCM) ambaye katika swali lake la nyongeza alitaka kujua hatua zinazochukuliwa kudhibiti urasimu wa wakurugenzi katika utolewaji wa fedha hizo.

Mbunge huyo pia alishauri ili urasimu huo udhibitiwe na makundi hayo mawili yasipate shida za kupata fedha hizo, mifuko hiyo iliyoko chini ya halmashauri lakini inayotengewa fedha na Serikali Kuu, iwe chini ya wabunge wa Viti Maalumu.

Akijibu maswali hayo, Jaffo alisema haina sababu mifuko hiyo isimamiwe na wabunge wa Viti Maalumu pekee kwa kuwa ni jukumu la viongozi wote wa halmashauri wakiwemo wabunge, madiwani na wakurugenzi kusimamia mifuko hiyo.

“Ni wajibu wetu wote kuisimamia mifuko hii. Naagiza wakurugenzi wote kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa kutoa fedha hizi ili zifikie walengwa,” alisema.

Katika swali la msingi la mbunge huyo, alitaka kufahamu ni akinamama na vikundi vingapi vya vijana vimenufaika na mikopo kupitia fedha za mifuko ya wanawake na vijana katika halmashauri za mkoa wa Iringa.

Akijibu swali hilo, Jaffo alisema katika mwaka huu wa fedha halmashauri za mkoa wa Iringa ziliwezesha vikundi vya wanawake 430 na vijana 47 kupata mikopo.

Alisema Halmashauri ya wilaya ya Mufindi iliwezesha vikundi vya wanawake 331, wilaya ya Kilolo vikundi vitatu, wilaya ya Iringa 73 na manispaa ya Iringa 23. Aidha, alisema jumla ya Sh milioni 339 zilitolewa kwa ajili ya mfuko wa akinamama na Sh milioni 98 kwa mfuko wa vijana mkoani humo.