23Mei2013

 

Benki ya Exim kuwawezesha wanawake

BENKI ya Exim ya Tanzania imeahidi kuendelea kuunga mkono uwezeshaji kwa wanawake katika maeneo mbalimbali nchini katika jitihada zake za kusaidia kukuza uchumi.

Meneja Masoko Msaidizi wa Benki ya Exim, Anita Goshashy alisema benki hiyo ilianzisha bidhaa za kipekee, zinazowalenga wanawake kwa kutambua umuhimu wao katika kuleta maendeleo.

Alisema hayo wakati wa kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, iliyodhaminiwa na Benki ya Exim jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Goshashy alisema uwezeshaji wa kiuchumi miongoni mwa wanawake, unasaidia katika kuchangia ukuaji wa uchumi nchini. Alisema ongezeko la fursa kwa wanawake linasaidia ujenzi mzuri wa familia, jamii na nchi nzima kwa ujumla.

“Uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake ni muhimu kama nchi inalenga kupata maendeleo ya kiuchumi yalio endelevu. Kwa kulitambua hili, Benki ya Exim ina bidhaa za kibenki kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake,” alisema Goshashy.

Goshashy alisema mpaka mwishoni mwa Desemba mwaka jana, benki hiyo ilitumia Sh bilioni 21 katika jitihada za kuwasaidia wanawake kupitia mpango wake wa kuwasaidia wanawake wajasiriamali, unaojulikana kama Women Entrepreneurs Financing Programme (WEF).

“Tumeamua kuwawezesha wanawake kwa sababu tunaamini wanawake wana nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo ya uchumi nchini,” alisema.

Alisema “Kama mwanamke atawezeshwa kiuchumi, Taifa litakuwa na uhakika wa kuwa na familia bora zitakazoweza changia maendeleo ya jamii na uchumi”.

Aidha, alisema kuwa benki yake pia imeweza kuwawezesha wanawake wanaojihusisha na biashara ndogo na za kati, kwa kuwapatia ujuzi mbalimbali wa kutengeneza biashara zenye faida na endelevu.

Awali, mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo, alitoa changamoto kwa wanawake kuwekeza katika kilimo, kutokana na kwamba sekta hiyo ina soko la uhakika.