Mfamasia anyima dawa wagonjwa, DC achukua hatua

WATU wawili wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) walioko kwenye dozi ya dawa za kufumbaza virusi hivyo (ARVs), wamenyimwa dawa hizo na kutupiwa vyeti vyao chini na kisha kufukuzwa na mfamasia mmoja katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, akijigamba kwamba ‘Hapa ni Kazi Tu.’

Wananchi hao ambao ni mwanamke mmoja na mwanamume mmoja, walifika hospitalini hapo wakiwa na vyeti vyao vinavyowatambulisha kuwa ni waathirika wa VVU na wako kwenye dozi, asubuhi na kumuona mfamasia huyo aliyetambuliwa kwa jina la Clyvanus Anthony Katula, ili wapate huduma hiyo ya dawa.

Kwa mujibu ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe, wagonjwa hao baada ya kumuona mfamasia huyo na kujieleza kwamba wako kwenye dozi ya dawa hizo (ARVs), mfamasia huyo aliwafokea akiwataka watoke mara moja hospitalini hapo.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao (majina yao yamehifadhiwa) ambao wote ni wakazi wa mkoa wa Lindi, walichukua hatua ya kumuona DC ofisini kwake na kutoa kero yao ya kunyimwa dawa hizo na mfamasia huyo.

DC Mirumbe pamoja na viongozi wengine akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, waliwachukua wananchi hao na kwenda moja kwa moja hospitalini hapo, ambako walimhoji mfamasia huyo.

Hata hivyo, mtuhumiwa huyo hakutoa majibu yoyote na ndipo Mkuu wa Wilaya ya Bunda alipoamuru uongozi wa hospitali hiyo kuwapatia dawa wananchi hao mara moja. Aidha, DC huyo alimwagiza daktari kiongozi wa hospitali hiyo kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi huyo wa umma pamoja na kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii juu ya kitendo alichokifanya mfamasia huyo ili hatua zaidi zichukuliwe dhidi yake kwa sababu haiwezi kasi ya Rais John Magufuli.