TFF isijidanganye na viwango Fifa

TANZANIA inashika nafasi ya 132 kwenye viwango vya ubora wa soka vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa(Fifa) kila mwezi. Hivyo ni viwango vya ubora vilivyotolewa mwezi huu na Tanzania kupanda kwa ubora huo kwa nafasi tatu, kwani ilikuwa ikishika nafasi ya 135.

Kwa mtazamo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na baadhi ya wadau wa soka hapa nchini haya ni mafanikio, kwani wamekuwa wakifanya jitihada sana kuona kwamba Tanzania inapanda kwenye viwango vya ubora vinavyotolewa na Fifa.

Ndio ni mtazamo wa TFF kwa muda mrefu sasa kuipandisha Tanzania kwenye viwango vya ubora wa Fifa na nyenzo yao kubwa mara nyingi imekuwa kuitafutia timu ya taifa mechi mbalimbali za kirafiki na nyingi kati ya hizo mechi zinachezwa kwenye Uwanja wa Taifa na lengo kuu ni kupanda kwa ubora baada ya mechi hizo.

Mabosi wa TFF na baadhi ya wadau wa soka hapa nchini mitazamo yao ni kwamba ili Tanzania ipande kwenye viwango vya ubora wa Fifa basi Taifa Stars ipatiwe mechi za kirafiki na baada ya mechi hizo ambazo mara nyingi wamekuwa wakitoka sare ni imani yao kuwa Tanzania inapanda.

Sijui, pengine vigezo vya kupanda kwa viwango vya ubora wa soka vinavyotolewa na Fifa ni kwa timu ya taifa kucheza mechi za kirafiki na kama ndivyo basi kwa hapa TFF inaweza ikawa sahihi sana katika hilo.

Ingawa sidhani kwa umakini wa Fifa pamoja na kashfa za ufisadi zinazolikumba shirikisho hilo ikaweka mechi za kirafiki kama kigezo pekee cha kupanda kwa ubora wa soka wa nchi yoyote duniani. Kama ndivyo hapa Fifa itakuwa imepotoka mchana kweupe.

Akili yangu inanituma kuamini kwamba siasa za soka za hapa nchini zinaifanya TFF kuchagua kipengele kimoja tu cha mechi za kirafiki ili kupandisha viwango vya ubora wa Fifa lakini katika uhalisia wake viwango vya ubora wa soka ni zaidi ya timu ya taifa kucheza mechi za kirafiki mara kwa mara.

Kuwepo na mipango ya kisayansi inayotekelezeka kwenye soka letu na tukifanikiwa katika hili mtazamo hautakuwa kupandisha ubora wa viwango vyetu kwa kucheza mechi za kirafiki tu bali kufanya vizuri kwenye mashindano yote kwani mifumo sahihi ndio uzao ubora wa soka sehemu yoyote ile duniani.

Kung’ang’ania kucheza mechi za kirafiki mara kwa mara na kupuuza mifumo sahihi ya kisayansi kukuza soka letu hakutatufanya tuwe na kiwango bora kinachotambulika na Fifa. Tanzania ni moja ya nchi zinazocheza mechi za kirafiki kwenye kalenda ya Fifa mara kwa mara lakini pamoja na kucheza mechi hizo imekuwa haifanyi vizuri kwenye mashindano makubwa kama vile kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia.

Hii inachangiwa zaidi na TFF kupuuza mifumo sahihi ya ukuzaji wa soka letu na kujikita zaidi kwenye kipengele kimoja tu cha kupata mechi za kirafiki ziliko kwenye kalenda ya Fifa na mechi hizo ni kwa timu ya taifa ya wakubwa pekee, Taifa Stars.