CHRISTINE LAGARDE: Awamu ya pili ubosi wake IMF yachanganya mataifa duniani

CHRISTINE Lagarde si jina jipya duniani, lakini huenda likawa jina kubwa la mwanamke mwaka ujao au pengine akawa mwanamke mwenye nguvu zaidi duniani, wakati atakapowania awamu nyingine ya kushika cheo chake cha sasa cha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Lagarde, ni mzaliwa wa Paris, Ufaransa ambaye alikwaa cheo hicho chenye madaraka makubwa ya kiuchumi duniani tangu mwaka 2011, lakini Julai mwakani anatarajiwa kumaliza miaka mitano ya uongozi wake huku akitajwa kutaka kuwania nafasi hiyo kwa awamu nyingine. Tayari nchi za Afrika zimeanza kulalamika kuwa umefika wakati wa kumaliza miaka 70 wa uongozi wa Shirika hilo, kutoka katika Bara la Ulaya pekee.

Msemaji mmoja wa Hazina ya Afrika Kusini ambaye hakutajwa jina, amenukuliwa akisema uongozi wa shirika hilo wa miaka 70 kutoka Bara Ulaya pekee, unapaswa kukoma. “Nchi zinazoendelea zinataka uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji mpya, uzingatie sifa za muombaji zaidi na kuepuka utaratibu wa sasa ambao Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo amekuwa akitoka Ulaya kila mara,” amenukuliwa msemaji huyo wa Afrika Kusini, ingawa malalamiko hayo ya Afrika yanaelezwa kuwa yamezoeleka na hayana jipya.

Hata hivyo ushindani mkubwa wa Lagarde katika kuwania awamu hiyo ya pili, unatajwa kutoka katika umoja wa mataifa yanayochipukia kiuchumi ya Brics, ambayo ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini. Kauli hiyo ya msemaji wa Afrika Kusini, kuonesha kana kwamba anaunga mkono msimamo wa Afrika, inatajwa kuwa udhaifu unaoweza kudhoofisha nchi hizo za Brics na kutoa fursa kwa Lagarde kupita tena.

Udhaifu mwingine umetajwa kutoka nchini China, ambako msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Hua Chunying, alisikika akisema wakati wa uongozi wa Lagarde, Shirika hilo na nchi hiyo zilikuwa na uhusiano mzuri. Hata hivyo baadhi ya wachumi wanasema kauli hiyo ya Hua, huenda imetokana na umuhimu wa Lagarde, katika kuunga mkono fedha ya China kuwa miongoni mwa fedha za kimataifa, ikiungana na Dola ya Marekani, Euro, Paund ya Uingereza na Yen ya Japan.

Taarifa zinaonesha kuwa India, inaweza kutaka kujadiliana na mataifa hayo ya Brics ili yajiunge pamoja kuhakikisha bosi mpya wa IMF, anatoka miongoni mwa nchi hizo. Taarifa hiyo iliungwa mkono na msemaji wa Wizara ya Fedha ya India aliyesema ni mapema kutoa jibu la moja kwa moja kuhusu nguvu ya mataifa ya Brics, mpaka hali halisi itakavyoanza kujionesha na wagombea watakapoanza kujitokeza.

Mataifa hayo ya matano ya Brics, ambayo yana uchumi unaotishia uchumi wa mataifa makubwa kiuchumi duniani, hasa ya Ulaya na Marekani, yameimarisha ushirikiano wao kwa lengo la kuanzisha Benki yao itakayoipa changamoto Benki ya Dunia na shirika lao la fedha, litakalotoa changamoto kwa IMF. Uamuzi wa mataifa hayo, umetokana na kukasirishwa kwao baada ya kukosa uwakilishi wa hadhi yao katika upigaji kura ya kufanya uamuzi ndani ya IMF, ambao China yenye uchumi mkubwa wa pili duniani pamoja na nchi hizo zingine nne, hazina kura zenye nguvu inayofikia hata robo ya kura za Marekani.

Hatua hiyo ya mataifa ya Brics, ilisababisha mtikisiko ndani ya IMF ambayo imekuwa ikijitahidi bila mafanikio kuweka uwiano sawa wa kura. Kuthibitisha mtikisiko huo, mtumishi wa pili kwa ubosi IMF, David Lipton, aliieleza Shirika la Habari la Uingereza (BBC) kuwa, anadhani Mkurugenzi Mtendaji ajaye atapaswa kutoka nje ya nchi za Bara la Ulaya. Sifa za Lagarde Waziri wa Marekani wa Fedha, Timothy Geithner, aliwahi kumuelezea Lagarde kuwa ni mcheshi, mtulivu na mwenye uwezo wa kujenga daraja penye migawanyiko.

Geithner anasema Lagarde amekuwa na sifa hizo katika uendeshaji wa IMF, huku akibaki kuwa mwaminifu katika kutetea maslahi ya Ufaransa katika siasa za kimataifa na sifa hizo zimekuwa zikimpa mvuto wa aina yake duniani. Wachumi wengi hawakuamiani, kuwa angeweza kukabiliana na tatizo la kufilisika la nchi ya Ugiriki na Ureno iliyokuwa ikinyemelewa na tatizo hilo, huku akikabiliana na mtikisiko wa uchumi duniani, lakini aliishangaza dunia katika kukabiliana na hali hiyo, jambo linalomuongezea sifa.

Historia yake Alizaliwa Januari 1, 1956 ni Mwanasheria na mwanasiasa kutoka chama cha Union for a Popular Movement na pia ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), tangu Julai 5, 2011. Alimrithi Dominique Strauss-Kahn na uteuzi wake ulizua maswali kwa kuwa alikuwa kiongozi wa 11 mfululizo wa IMF kutoka Bara Ulaya. Kabla ya hapo aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uwaziri katika nchi yake. Alikuwa Waziri wa Masuala ya Uchumi, Fedha na Ajira.

Pia aliwahi kuwa Waziri wa Kilimo na Uvuvi na Waziri wa Biashara. Amekuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi nyeti ya Fedha katika Jumuiya ya Nchi Nane Tajiri duniani (G8) na mwanamke wa kwanza kuongoza IMF. Aliwai pia kuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Kampuni ya Kimataifa ya Sheria Baker & McKenzie na Nevemba 16, 2009, Jarida la Financial Times, lilimteua kuwa Waziri Bora wa Fedha katika Ukanda wa Ulaya.

Mwaka huu unaokwisha, Lagarde ametajwa Jarida la Forbes kuwa mwanamke wa nne duniani kwa kuwa na nguvu kubwa za ushawishi. Historia yake Lagarde amezaliwa Paris, Ufaransa katika familia ya wasomi. Baba yake Robert Lallouette, aliyekuwa Professor wa Lugha ya Kiingereza na mama yake, Nicole, alikuwa mwalimu wa lugha ya Kilatini.

Yeye na kaka zake watatu walilelewa katika mji wa Le Havre na alipokuwa msichana, alikuwa mchezaji katika Timu ya Taifa ya Kuogelea ya Ufaransa. Akiwa na umri wa miaka 18, alishinda katika mchujo wa kupata nafasi ya kwenda kusoma katika Shule ya Wasichana ya Holton, iliyopo Bethesda, Maryland. Baadaye alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Paris X na kupata Shada ya Uzamili katika Kiingereza, Sheria za Kazi na Sheria za Jamii.

Alichukua pia Shahada ya Uzamili Mambo ya Siasa katika Chuo cha Sayansi ya Siasa cha Ufaransa. Ni mtumiaji wa vyakula vya mboga (vegetarian), hapendi kutumia pombe. Pia ni mpenzi wa kufanya mazoezi katika gym, kuendesha baiskeli na kuogelea, kupika na kutengeneza bustani za maua. Amewahi kuwa mshindi wa mashindano mbalimbali ya kuogelea na amekuwa akivutia sana wanaume, kwa namna anavyojiweka na amekuwa akifurahia namna anavyoelezewa alivyo na mvuto kwa wanaume.

Ni mwanamke anayependa kuvaa vizuri na ana uwezo mzuri wa kuishi maisha ya watu wa Marekani. Anazungumza Kiingereza kizuri bila makosa makosa na anapenda kuonekana kiwa na mvuto wake. Siasa Lagarde anapenda siasa, kwani alivyokuwa chuo kikuu, aliwahi kuwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Serikali ya Chuo, William Cohen, ambaye alikuja kuwa Waziri wa Ulinzi katika Serikali ya Marekani chini ya Rais Bill Clinton.

Anaelezewa kuwa amekuwa akipenda kushindana na wanaume na mara kwa mara alipoulizwa kuhusu tabia hiyo, alisema anachukia kusikia kuwa kuna namna ya kike na kiume ya kuongoza, kwa kuwa kila mtu ametokana na mwanamke na mwanamume. “Wanawake viongozi wana uwezo mkubwa wa kuwa wasikivu na wanaopenda ushirikiano na kuonesha kujali kwa wanaowaongoza kuliko wanaume,” anasema.

Mwaka 1968, wakati kulipotokea mgomo katika shule za Ufaransa kwa nchi nzima, ambapo wanafunzi waliandamana na kurusha mawe kwa askari Polisi waliokuwa wakilinda usalama, Lagarde alikwenda kufanya mazoezi ya kuogelea.