Lucy Ngowi

SHIRIKA la Kimataifa la Uhamiaji limeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ukimwi kwa kuzungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kwa kutoa elimu ya Ukimwi.

Wakati wa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi hao wa Muhimbili, Ofisa Miradi wa Shirika hilo, Charles Mkude aliwaeleza jinsi ambavyo wahamiaji wanaweza kuwa na mchango katika suala zima la Ukimwi.

Alisema waliwaeleza wanafunzi hao, kile ambacho shirika linafanya kuhusu masuala ya Ukimwi, pia kulikuwepo na watoa mada wengine kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) na wahadhiri chuoni hapo.

Alisema shirika hilo wamefanya utafiti katika ukanda wa usafiri wa masafa marefu kutaka kujua madereva wana vituo vingapi wanaposimama na pia wanafanya nini wanapokuwa wamesimama huko njiani.

Mkude alisema katika utafiti huo, waliangalia wao kama shirika wanaweza kutoa huduma zipi kwa madereva hao na kuwaelimisha juu ya maambukizi ya Ukimwi ili nao waweze kuelimisha jamii wanaposimama huko njiani badala ya kushawishika kufanya mambo mengine.

Alisema endapo madereva watakuwa na uelewa kuhusu elimu ya Ukimwi wanaweza kuisambaza kwa wengine.

Dk Sweetbert Kamazima ambaye ni Mhadhiri wa masuala ya Sayansi ya Tabia za Binadamu, alisema kila mwaka chuoni hapo wanasherehekea Siku ya Ukimwi.