Mfanyabiashara achinjwa Maswa

MFANYABIASHARA mmoja, Robert Dwese (43), mkazi wa Biafra Maswa Mjini ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na usoni na kufa papo hapo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Simiyu, Gemin Mushy alisema kuwa tukio hilo la kinyama lilitokea juzi majira ya saa 2:00 usiku eneo la Mnadani katika kata ya Nyalikungu katika tarafa ya Nunghu mjini Maswa.

Akifafanua juu ya tukio hilo alisema kuwa mtu au kundi la watu wasiojulikana walimshambulia mtu huyo maarufu kwa jina la “Masanja” ambaye ni mfanyabiashara wa mifugo na kisha kutokomea kusikojulikana.

Jeshi la Polisi mkoani hapa limeanza upelelezi na uchunguzi kuwabaini watu waliohusika katika mauaji hayo na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji. Hilo ni tukio la kwanza kutokea katika eneo hilo likimhusisha mfanyabiashara wa mifugo mjini humo.