Kocha aizungumzia sare ya Azam kwa JKT Ruvu

KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Dennis Kitambi amesema sababu ya timu yao kufanya vibaya katika mechi za karibuni ni wachezaji wao kukosa ari ya kupambana hasa wanapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Azam juzi ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, ilijikuta ikipoteza kabisa matumaini ya ubingwa baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2, na JKT Ruvu licha ya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kitambi alisema kukosa umakini kwa wachezaji wao ndiko kulikowapa JKT Ruvu nafasi ya kusawazisha mabao yote mawili na kupata sare hiyo ambayo imepoteza kabisa matumaini ya ubingwa.

“Asilimia kubwa ya wachezaji wetu wamepoteza ari ya mwendelezo wa ushindi na ndiyo sababu tumekuwa tukipata matokeo mabaya hasa tunapocheza nyumbani, kwa sababu kama makocha tulizungumza nao wakati wa mapumziko tukiwa mbele kwa mabao 2-0, kuhakikisha tunafunga bao la tatu kipindi cha pili ili tupumzike, lakini imekuwa tofauti,” alisema Kitambi.

Kocha huyo alisema kama makocha wanaumizwa na matokeo mabaya, lakini watajipanga kuhakikisha wanashinda mechi zao zilizosalia ili waweze kumaliza kwenye nafasi ya tatu. Naye kocha wa JKT Ruvu, Abdallah Kibadeni alisema pamoja na kupata sare hiyo, mchezo ulikuwa mgumu kwa upande wao na aliwapongeza wachezaji wake.