Tusiponde kila jambo la TFF

WATANZANIA tumekuwa na tabia nyingi za ajabu ambazo hatukuwa nazo na wala haijawahi kuwa desturi tangu kuumbwa kwa dunia.

Lakini kadri siku zinavyoenda mbele tabia zinabadilika sana na imefikia hatua tuseme wazi kwamba tunakoelekea siko kabisa na kuna haja tena ya makusudi ya kubadilika na kurejea zamani ambako mila na desturi zetu zinatuelekeza.

Tabia mbaya ni nyingi na visingizio vyake ni vingi hali kadhalika, nikisema nizioredheshe hapa hapatatosha kabisa, lakini kwa uchache ni uasherati uliokithiri, uvaaji wa mavazi ya kuonesha uwazi mkubwa wa maungo hasa akina dada, usagaji, ushoga, utapeli, wizi na mengineyo.

Lakini kuna gonjwa kubwa pia ambalo linahusu utoaji wa maoni katika kada tofauti hata kama huna uelewa au ujuzi wa kutosha wa jambo hilo kwa kisingizio cha uchambuzi au uandishi.

Binafsi naamini sana kwamba uandishi wa habari au uchambuzi ni kada inayotaka weledi kama zilivyo kada nyingine mbalimbali na wala si sehemu ya kulipa visasi, kuanzisha ugomvi, kupinga usilolipenda au kuafiki kwa maslahi binafsi, kuendeleza mapambano au chochote ambacho hakina tija kwa maendeleo ya wengi au Taifa.

Ila ni sehemu ya kusema ukweli ukiwa na ufahamu na uthibitisho wa kutosha juu ya unalotolea uchambuzi au unaloandikia makala yako husika bila kujali upande ila ukiweka maslahi ya wengi na taifa mbele, na wala si kama ilivyo sasa.

Kuna wimbi la uchambuzi na wachambuzi na waandishi wa zinazoitwa makala katika fani na kada mbalimbali nyingi kwa mtazamo wangu zikiwa zinapotosha jamii ama kwa makusudi au bila kukusudia.

Kuna ambao jamii inawaamini sana, kiasi cha kwamba wapo watu ambao huamini kila wanalosoma kupitia wao au kusikia na kuufanya ndio msingi wa mazungumzo yao kila waendako na wanapotaka kukosoa au kusifia lolote hutumia chambuzi zao kama vigezo.

Binafsi huwa naumia sana ninaposoma mahali kuhusu mambo ya soka, huku mchambuzi au mwandishi akitoa takwimu zisizo za kweli au akielezea kitu ambacho unaona kabisa aidha hajui au hana uelewa nacho kiasi cha kutosha. Lakini pia huwa nafurahi kupita maelezo ninapoona mtu akiandika kitu ambacho kina ukweli na anafahamu kile anachotolea uchambuzi.

Hapo ndipo ninamthamini na kumwamini huyo mchambuzi au mwandishi. Katika soka la nchi hii kuna kaumu ya wachambuzi na waandishi wa mambo ya kandanda ambao wana sifa zinazotofautiana kwa namna mbalimbali.

Ndani yake ni wale wenye weledi na wamejijengea heshima kunako jamii yetu, kwa usahihi wa kile wanachotolea uchambuzi na kuna ambao hata ukisoma chambuzi zao, unajua hapa kuna kasoro nyingi na wala hakuna mchambuzi ila kuganga njaa tu.

Kuna mijadala mingi kuhusu soka letu tangu kuondoka kwa utawala wa Leodegar Tenga na kuingia huu wa Jamal Malinzi. Lakini namna mijadala inavyoendeshwa ni kama vile si kwa ajili ya kujenga soka letu bali ni kuangalia upi ulikuwa upande wako wakati wa uchaguzi, basi unaanza aidha kusifia sana au kukosoa hata usivyovielewa na hatimaye unapotoka.

Hii imekua tabia ya wachambuzi wetu kutafuta upande wa kuukosoa sana na ule wa kuupendelea hata kwa mabaya, na hapa ndipo mimi naona ni tabia ya ajabu kama zile nilizozitaja awali. Binafsi nashindwa kujua mtu anatoa maoni au uchambuzi wake unasimamia hapo kwa hoja dhaifu.

Unajiuliza huyu anajua anachokisema au anaropoka tu? Kuna mwingine aliwahi kusema kwamba vipaji havisakwi kama ndezi au swala mwituni! Watanzania tumejaaliwa maneno ya hovyo banaa. Uchambuzi au uandishi wa makala za soka na habari zake ni zaidi ya kutumia uzoefu wa kwenda kiwanjani tu, unahitaji kujibidiisha katika maeneo mengine jamani.

Kinyume chake kama una tatizo na takwimu za kitu fulani ni vyema na heri ukiuliza ili kujiridhisha na wala sio kama tunavyofanya. Natumaini sitakuwa adui kwa kusema ukweli.

*Mwandishi wa makala haya ni mchezaji wa zamani wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara na amepata kuchezea Taifa Stars, ambapo pia ana taaluma ya ukocha. Kwa sasa ni Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).