Serikali yajipanga kupunguza kesi mahakamani

KATI ya mashauri 250 yaliyofunguliwa mahakamani ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa majimbo na kata uliofanyika Oktoba mwaka jana, mashauri 28 yote ya ubunge yamehitimishwa hadi kufikia Aprili mwaka huu.

Kati ya kesi hizo zilizofunguliwa mahakamani, 52 ni za ubunge na 198 ni za udiwani. Kesi hizo 28 zilizohitimishwa ni za ubunge na 24 bado zinaendelea.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema hayo wakati anawasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2016/2017, alisema katika kesi zote hizo ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ambayo inaendesha kesi hizo ilishinda na kufanya wabunge wote walioshinda kuendelea na ubunge wao.

Akizungumzia mikakati ya serikali katika kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani, alisema mahakama zimejiwekea utaratibu wa kumaliza mashauri yote yaliyopo mahakamani katika mwaka ujao wa fedha yenye umri wa zaidi ya miaka miwili kwa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Waziri Mwakyembe alisema mpango huo umeanza kuonesha matunda ambapo jumla ya mahakama za mwanzo 128 kati ya 906 zilizoko nchini, zimesikiliza na kutolea uamuzi mashauri yote yaliyofunguliwa katika mahakama hizo kati ya Januari na Desemba mwaka jana.

Kwa upande wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017 iliyosomwa na Makamu Mwenyekiti wake, Najma Giga ilitaka Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhuisha mchakato wa kupata Katiba mpya kutokana na mapendekezo yaliyotolewa katika mchakato wa kupata katiba uliosimama Oktoba mwaka 2014.

“Kamati inasisitiza ni muhimu kwa serikali kutenga fedha au kuongeza fedha ya nyongeza katika mwaka huu wa fedha ili kumalizia mchakato wa Tanzania kupata katiba mpya,” alisema.