Vifo vya matatizo ya uzazi kutolewa taarifa

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakusudia kutoa taarifa ya wanawake wanaofariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi kila baada ya miezi mitatu ili kukabiliana na tatizo la vifo vya wanawake nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu juzi jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Viongozi Wanawake katika masuala ya Afya.

“Nimeamua kuhakikisha wanawake wanapiga hatua na kuthaminiwa katika jamii, kwa kuanzia na kutoa ripoti ya robo mwaka kwa kila halmashauri kuhusu taarifa ya wanawake wanaofariki kutokanana matatizo ya uzazi,” alisema.

Waziri Ummy alieleza kuwa katika uteuzi atakaofanya kwenye bodi zilizo chini ya wizara yake, atahakikisha asilimia 30 ya wajumbe wa bodi hizo ni wanawake.

Baadhi ya Bodi zilizo chini ya Wizara yake ni pamoja Bohari ya Dawa (MSD), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Bodi ya Wafamasia.