Rais wa Chama Cha Madaktari kizimbani
- Imeandikwa tarehe 11 Julai 2012
- By Regina Kumba
- Imesomwa mara: 1408
RAIS wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na mashitaka ya kukaidi amri ya Mahakama iliyozuia mgomo wa madaktari na kuhamasisha mgomo wa madaktari kinyume cha sheria.
Â
Dk Mkopi alisomewa mashitaka jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi, Faisal Kahamba.
Awali kabla ya Dk Mkopi kupandishwa kizimbani, tangu saa 2 asubuhi madaktari walifurika kwenye Mahakama ya Kisutu na ilipofika saa 3.45 asubuhi mshitakiwa huyo aliletwa mahakamani akiwa kwenye gari la Polisi Toyota Land Cruiser namba T 671 BEQ.
Dk Mkopi alidaiwa kuwa kati ya Juni 26 na 28 Dar es Salaam, akiwa Rais wa MAT hakutii amri iliyotolewa Juni 26 na Mahakama Kuu Tanzania, Kitengo cha Kazi.
Amri hiyo ilimtaka Dk Mkopi atangazie wanachama wake kwamba wamezuiwa kushiriki mgomo kama amri ya awali iliyotolewa na Mahakama Juni 22.
Katika mashitaka ya pili ilidaiwa kuwa Juni 27, Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa mjumbe wa MAT alishawishi wajumbe wa chama hicho kufanya mgomo kinyume na amri ya Mahakama.
Hata hivyo Dk Mkopi alikana mashitaka yote na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Mawakili wanaomtetea, Isaya Matamba, Dk Maulid Kikondo, Dk Gaston Kennedy na Dk Rugemeleza Nshala waliomba dhamana kwa mteja wao ambapo upande wa mashitaka haukuwa na pingamizi.
Hakimu Kahamba aliweka masharti ya mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya Sh 500,000. Kesi hiyo itatajwa Agosti 6.


