Fedha za BRN kuboresha vituo vya afya Ukerewe

HALMASHAURI ya wilaya Ukerewe mkoani Mwanza inaendelea kuboresha miundombinu ya zahanati na vituo vya afya baada ya fedha kutoka serikali kuu kupitia mpango wa matokeo makubwa sasa BRN.

Mkuu wa wilaya ya Ukerewe, Estomiah Chang’ah amesema kupatikana kwa fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 300 kutaboresha miundombinu katika vituo vya afya na zahanati hasa vijijini na kutoa fursa nzuri ya kutoa na kupata huduma katika mazingira mazuri.

Aidha alisema ujenzi wa vyumba vya kisasa vya upasuaji katika vituo vya afya Muriti na Kagunguli umekamilika na baada ya muda mfupi vitaanza kufanya kazi hivyo kuondoa tatizo la wahitaji kufuata huduma mbali.

“Ndugu zangu wakazi wa kijiji cha Muriti, shirika la AMREF limetoa fedha nyingi kutekeleza mradi huu, ambao pamoja na kusogeza huduma karibu pia utaokoa maisha ya wajawazito,” alisema Chang’ah.

Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Ukerewe, Dk Sadick Mtoigwa alisema vituo vya afya vitatu na zahanati zote 28 za wilaya hiyo kila moja imepata Sh mil. 10 kwa ajili ya kuboresha miundombinu.

Alisema fedha hizo zimetolewa na serikali kupitia mpango wa matokeo makubwa na hadi sasa wanaendelea kukamilisha shughuli za kurabati majengo kwa kupaka rangi, kurudishia miundombinu iliyoharibika kama milango, madirisha na kujenga vyoo.

Aidha Dk Mtoigwa amesema AMREF imetoa Sh 373,076,765 kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha upasuaji katika kituo cha afya muriti wakati kituo cha afya Kagunguli kimepata Sh 347,084,315 za shughuli kama hiyo.

Alisema shughuli ya ujenzi wa vyumba vya upasuaji katika vituo hivyo vya afya umekamilika na baada ya muda wa miezi miwili wanatarajia kuanza kutoa huduma.