Wazazi wasioandikisha watoto kushitakiwa

MKUU wa wilaya Kibondo mkoani Kigoma, Louis Bura ametangaza kiama kwa kuwachukulia hatua ikiwemo kuwapeleka mahakamani wazazi watakaoshindwa kuwaandikisha na kuwapeleka watoto wao shule hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu.

Bura amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa ujenzi wa madarasa katika shule za msingi wilayani humo kuondoa tatizo la madarasa linalokabili wilaya hiyo.

Uzinduzi uliofanyika shule ya msingi Ngamruguma wilayani Kibondo. Mkuu huyo wa wilaya alisema hakuna sababu yoyote itakayokubalika itakayotolewa na mzazi kueleza kwamba hakumpeleka mtoto wake kuanza masomo ya darasa la kwanza sambamba na wale wa kidato cha kwanza.

Aidha Bura amesema wakati serikali ya wilaya ikitekeleza mpango wa kuondoa upungufu wa madarasa katika wilaya hiyo hatakubali kuona baadhi ya wananchi wachache wanakwamisha utekelezaji wa mpango huo wa kuondoa upungufu wa madarasa wilayani humo, kwa sababu yoyote ikiwemo itikadi za kisiasa.

Kwa sasa alisema uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza uko chini ya asilimia 30 na kwamba katika shule za sekondari serikali itafanya sensa na kufuatilia wanafunzi wote waliofaulu ambao hawajaripoti katika shule walizopangiwa.

Awali akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kibondo, Juma Mnwele alisema hadi sasa wilaya hiyo inakabiliwa na upungufu wa madarasa 138 katika shule zake 28 za msingi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.3 zinahitajika huku baadhi ya shule zikilazimika kutumia madarasa ya shule nyingine kwa ajili ya wanafunzi kusomea.

Kutokana na hilo, alisema kuwa mpango huo wa uhamasishaji utakuwa ukifanyika mara mbili kwa wiki kwa kila shule ambapo wakuu wa idara na watendaji wa halmashauri na ofisi ya Mkuu wa Wilaya watakuwa vijijini wakishiriki kwenye miradi ya ujenzi wa madarasa huku wananchi wakipaswa kuchangia mawe, mchanga na kokoto kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo.