DC Ukerewe aitwa Mpanda kwa kutokamilisha miradi

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi wameiomba Serikali imrejeshe aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Esthom Chang’a ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya, na aliyekuwa Mhandisi wa Maji, Resicipie Leo ili wasimamie ujenzi wa miradi miwili ya maji ambayo hawakuikamilisha.

Miradi hiyo ni ya thamani ya zaidi ya Sh milioni 152 na wametakiwa kurejesha fedha hizo kwani wakandarasi hawapo na miradi haijakamilika wakati walilipwa fedha yote.

Hatua ya kutakiwa kurejesha fedha imependekezwa na Kamati ya Fedha na Mipango na wametakiwa wazirudishe katika halmashauri hiyo fedha zote zilizotumika kuwalipa wakandarasi ambao wameshindwa kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo miwili ya maji, kwa kuwa fedha hizo ni za halmashauri hiyo.

Chang’a kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza na Leo alihamishiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma. Ilielezwa kuwa katika kipindi chao cha uongozi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, waliwalipa wakandarasi fedha zote huku ujenzi wa miradi hiyo miwili ya maji ikiwa haijakamilika.

Uamuzi huo ulifikiwa na madiwani hao katika kikao chao cha Baraza la Madiwani kilichoketi mjini hapa jana, kilichoongozwa na Mwenyekiti wake, Hamadi Mapengo.

Mwenyekiti Mapengo akifungua kikao cha baraza hilo, alieleza kuwa Kamati ya Fedha na Mipango ya halmashauri hiyo ilibaini kuwa ujenzi wa miradi miwili ya maji katika shule za sekondari za Mpanda Ndogo na Kabungu zenye jumla ya thamani ya Sh milioni 152 haukukamilika licha ya wakandarasi wake kulipwa fedha zote na kuondoka.

Akifafanua, Mapengo alieleza kuwa ujenzi wa mradi wa maji katika shule ya sekondari ya Mpanda Ndogo umegharimu Sh milioni 72 na wa shule ya sekondari Kabungu uligharimu Sh milioni 80 na yote haijakamilika ujenzi wake.

“Kamati ya Fedha na Mipango ilipendekeza Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Chang’a na Mhandisi wa Maji, Leo aliyehamishiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kikazi wote warudishwe waje kujieleza ni kwa nini waliwalipa wakandarasi waliokuwa wakijenga miradi hiyo ya maji fedha zote bila kukamilisha ujenzi wake. Mbaya zaidi fedha hizo ni za halmashauri yetu. Hivyo kamati imependekeza wawili hao warudishwe ili wasimamie ujenzi wa miradi hiyo hadi ikamilike tena kulingana na thamani ya fedha iliyokuwa imetengwa au wazirudishie fedha zote walizowalipa wakandarasi hao,” alisema Mapengo.

Alisema kuwa tayari halmashauri hiyo imeshamwomba kwa maandishi Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi aandike barua kwa mamlaka husika ya kuomba Leo arudishwe katika halmashauri ya Mpanda kujibu tuhuma hizo.

Wakichangia mapendekezo hayo, diwani wa Karema, Maiko Kapata, alilieleza baraza hilo kuwa kumekuwa na tabia ya wataalamu wa halmashauri hiyo kuwapa majibu ya kuwadanganya madiwani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya mpya ya Tanganyika, Salehe Mhando, alisisitiza akiwa msimamizi mkuu wa halmashauri hiyo atahakikisha kila senti ya halmashauri hiyo inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na yeyote atakayezifanyia ubadhirifu hatasita kuhakikisha anachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo kuburuzwa mahakamani.