Trafiki waanza kukamata gari zenye taa za mwanga mkali

MKUU wa Kitengo cha Elimu, Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mossi Ndozero, amesema kwamba ukamataji wa magari yaliwekwa taa za mwanga mkali umeanza na utaendeshwa nchi nzima.

Akizungumza jana na gazeti hili, Mossi alisema wanafanya ukamataji huo kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani sura ya 168 (39) iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

“Hili ni operesheni ya nchi nzima ndio maana aliyetoa tamko hilo ni Mkuu wa Trafiki Tanzania,” alisema Mossi na kuwataka wale ambao wameweka taa hizo kwenye magari yao kuziondoa mara moja.

Alisema tayari ukamataji huo umeanza katika mikoa ya Dar es Salam na mikoa mingine.

”Hapa sina takwimu rasmi ila ukamataji umeshaanza katika mikoa ya Dar es Salaam, Ruvuma na Kilimanjaro na katika mikoa mingine ambayo kwa hapa nilipo siwezi kuitaja maana niko nje ya ofisi.”

Mkazi wa Moshi, Mohamed Suleiman ni mmoja wa watu waliopatikana na makosa kama hayo. Alikamatwa juzi na polisi wa usalama barabarani na kuandikiwa kosa la kufunga taa za mwanga mkali kwenye gari lake na kuandikiwa faini ya Sh 30,000.

“Uwekaji wa taa hizo ni kinyume cha sheria ya usalama barabarani kifungu cha 39 sura ya 168 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002,” alisema Mossi.

Polisi imepiga marufuku uwekaji huo wa taa za urembo kwenye magari huku tayari wafanyabiashara wanaouza vipuri vya magari wameziagiza kwa wingi.

Tamko hilo la Mpinga ni wazi kwamba litawafanya wafanyabiashara hao wasiuze vipuri hivyo.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga hivi karibuni alisema utekelezaji wa operesheni hiyo unatokana na katazo alilitoa Desemba 22 mwaka jana.

Mpinga alisema madereva watakaokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria, kwani tayari maelekezo yametolewa nchi nzima.