Watakiwa kujiunga na Kituo cha Kumbukumbu

SERIKALI imezitaka taasisi za umma, sekta binafsi na wafanyabiashara kujiunga katika matumizi ya Kituo cha Kutunzia Kumbukumbu (IDC) kwa ajili ya kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuchochea maendeleo na kukuza uchumi.

Aidha, kituo hicho kitasaidia kutunza siri za ndani ya nchi tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna matumizi makubwa ya mitandao ya nje ambapo siri hazitunzwi ipasavyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Naibu Waziri, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema kuwa serikali na taasisi kwa ujumla zinauhitaji mkubwa wa kutumia kituo hicho kwa kuwa zinajihusisha na ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi na utoaji wa data.

Ngonyani alisema taasisi hizo ambazo zinauhitaji mkubwa wa kutumia kituo hicho ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili wa Vizazi na Vifo (RITA) na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA).