NIC kuwezesha bima ya moto shule za serikali

SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC), limesema limejipanga kuisaidia serikali mzigo mkubwa inayoupata majanga yanapotokea kwa kujikita kutoa kinga dhidi ya moto kwa ajili ya shule ambazo zikiungua serikali inapata mzigo mkubwa kuijenga tena.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Bima za Maisha na Pensheni wa shirika hilo, Michael Mowo alisema NIC kama taasisi ya serikali inatoa kinga za bima kwa majanga mbalimbali yanayozunguka jamii ikiwemo majanga ya moto, wizi, ajali na kifo.

Alisema maisha yamezungukwa na majanga kadri ya mazingira yalivyo, hivyo NIC inatoa huduma za bima kwa ajili ya wananchi na kutoa fidia kwa pengo la kipato au ulemavu na kifo utakaokuwa umetokana na majanga mbalimbali yatakayobainika yamempata mwananchi na mali zake.

Alizitaja faida wananchi wanazopata kutoka NIC kwa mpango huo wa kutoa huduma za bima ni pamoja na kutoa fidia kwenye majanga tofauti yaliyowapata wananchi kwa uharaka.

Alisema fidia kwa waathirika ambao ni wananchi NIC inatoa bima za maisha kukinga majanga ya vifo kwa walengwa na mbima analipwa pesa yake na faida inayopatikana akifa mwisho wa mkataba.

Aidha alisema zipo bima za elimu, afya, matumaini na bima za vikundi ambazo ni faida kwa watanzania kwani janga la kifo likitokea ndani ya mkataba warithi wa mbima wanafidiwa kima cha bima bila kujali alichanga muda gani.

Hata hivyo, alisema NIC imekuwa ikitoa elimu ya bima kwa wananchi na kusisitiza kwamba huduma za bima za NIC zinalenga watanzania wote hasa wale wa kawaida.

Pia alisema shirika limejikita kuboresha huduma zake ili mtanzania wa kati aweze kufaidi matunda ya bima.