Mukangara kuondoa kero ya maji

MGOMBEA wa nafasi ya ubunge wa jimbo la Kibamba kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Fenella Mukangara amezindua kampeni zake za ubunge kwa kuahidi kukabiliana na kero ya maji.

Mgombea huyo alizindua kampeni zake hizo katika eneo la Kimara Mwisho. Mkutano ambao ulihudhuriwa na maelfu ya watu. Akitaja vipaumbele vyake, Dk Fenella alisema anatambua ukubwa wa kero ya maji kwa jimbo hilo na ameshaanza jitihada za kutatua kero hiyo.

Alisema kuwa atajenga tangi kubwa la maji, litakalohifadhi maji yanayopita jimboni hapo kutokea Mto Ruvu na kuyatiririsha katika mabomba mengine yanatayofika kwa wananchi. Pia, alisema ameshachimba visima katika kata mbalimbali kama vile Kibamba, Mbezi na Salange, ambavyo ni vikubwa na virefu vinavyotoa maji mengi.

Alisema kuwa kero hiyo ya maji ni ya muda mrefu katika jimbo hilo na inahitaji watu mahiri wa kuitatua na kuongeza kuwa amejipanga kuwasaidia wakazi hao katika sauala hilo.

Akizungumzia zaidi mkakati wake katika kukabiliana na kero hiyo, alisema kuwa tayari yapo mabomba ya maji katika eneo la Kwembe na kinachotakiwa ni ufuatiliaji ili kuhakikisha yanatumika kusambaza maji ambayo atayaleta.

Alisema kuwa kero hiyo imekuwa ikiwasumbua watu wengi, hasa akina mama kwa kuwa ndio wanatembea umbali mrefu kuyatafuta. Pia alizungumzia mkakati wake katika kutatua kero za Afya katika jimbo hilo. Alisema licha ya jimbo la Kibamba kuwa na watu wengi, lina changamoto ya uhaba wa zahanati za afya.

Alisema kuwa atashirikiana na wananchi katika kuhakikisha kuwa zinajengwa zahanati tatu katika kata za Kimara, Mbezi na Kibamba na kila moja kuwa itapewa gari maalumu la kubeba wagonjwa.

Alisema wananchi wanatembea umbali mrefu kutafuta zahanati na kuwa hakuna zahanati za kutosha na aliwataka wananchi hao kumchagua ili atatue kero hiyo. Dk Fenella pia alizungumzia mkakati wake wa kutatua kero ya ajira kwa vijana na kuwasaidia akinamama kukabiliana na kero ya umasikini, ambapo alisema kuwa ataunda kambi kazi katika kila kata.

Alisema katika kambi hizo vijana watapewa mafunzo maalumu ya ujasiriamali, ikiwa ni pamoja na kufundishwa namna ya kutumia fursa zinazowazunguka. Alisema kuwa ili kuhakikisha kuwa anawajengea njia mbadala za kujiajiri, atahakikisha kuwa kinajengwa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (Veta) katika jimbo hilo.