Kamati yamuonya Duni

KAMATI ya Maadili ya Kitaifa imetoa onyo kali kwa mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Juma Duni Haji, kwa kutoa taarifa zisizo sahihi kwa umma, akidai kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeongeza vituo hewa vya kupigia kura.

Aidha, kamati hiyo katika taarifa yake iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Hamid, imemtangaza Duni kuwa amekiuka maadili ya uchaguzi kwa kuudanganya umma kwamba tume imeongeza vituo hewa zaidi ya 20,000.

“Kamati inatoa onyo kali kwa Ndugu Juma Duni Haji kutorudia kutoa taarifa zisizo sahihi kwa umma,” ilisema taarifa hiyo iliyokwenda sanjari na barua aliyoandikiwa mgombea huyo, akiambiwa atakaporudia, kamati itachukua hatua kali zaidi dhidi yake.

Uamuzi huo wa kamati unatokana na malalamiko yaliyowasilishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu uvunjaji wa Maadili ya Uchaguzi ya Mwaka 2015, uliofanywa na mgombea huyo.

Kikao cha maadili kilichofikia uamuzi wa kumuonya mgombea huyo, kilihudhuriwa na wajumbe kutoka vyama mbalimbali vya siasa chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu mstaafu, Hamid. Wajumbe wengine ni Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, Katibu wa Kamati, Emmanuel Kawishe pamoja na wawakilishi wa vyama vya siasa.

Miongoni mwa wajumbe na vyama vyao vya siasa kwenye mabano ni Kahaliki Jumapili (ADC), Eugene Kabendera (Chaumma), Soud Rajab (ACT-Wazalendo), Felix Makuwa (UPDP) na Steven Kazidi (CCM), Dominata Rwechungura (TLP), Hassan Almas (NRA) na Irene Kadushi (SAU).

Duni alilalamikiwa kwamba, katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma, Oktoba 7, mwaka huu na katika mkutano wa kampeni za uchaguzi, Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, alitoa kauli isiyo sahihi na ambayo hajaithibitisha kinyume cha kifungu cha 2.1 (d) na 2.2 (h) vya Maadili ya Uchaguzi.

Barua ya Tume kwenda kwa Mwenyekiti Kamati ya Maadili Taifa, ilisema Duni alidai Tume ya Uchaguzi ni wezi na imetenga/kuongeza vituo hewa zaidi ya 20,000 vya kupiga kura.

Ililalamika kwamba, kurudiwa kwa kauli hiyo hata baada ya ufafanuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi, inaonesha dhamira ya Duni kuwa na nia ya makusudi ya kupotosha umma kwa kauli zisizo za ukweli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Maadili ya Kitaifa juu ya uamuzi kuhusu suala hilo, Duni aliandikiwa barua na Katibu wa Kamati ya Maadili kujulishwa malalamiko hayo na alipewa nakala ya barua ya malalamiko na ushahidi wa maandishi pamoja na video lakini hakujibu na wala kufika kwenye kikao cha kamati licha ya kukiri kupokea barua.

“Kamati iliamua kuanza kikao na kujadili malalamiko hayo. Kwa kuwa Chadema waliidharau, Kamati ya Maadili ya Kitaifa imefikia maamuzi ya kumwadhibu ndugu Duni Haji kwa kuzingatia kifungu cha 5.10 (b) na (c) cha Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015 ambayo Chadema waliyasaini kama vyama vingine,” ilisema taarifa hiyo.