21Mei2013

 

Kesi ya akina Iddi Simba yaahirishwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo imeahirisha kumsomea maelezo ya awali Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) Ltd, Iddi Simba na washitakiwa wenzake wanaokabiliwa na mashitaka ya kula njama, kughushi, kuchepusha fedha na kusababisha hasara ya Sh bilioni 2.4.

Kesi hiyo ambayo Simba ameshitakiwa pamoja na meneja wake, Victor Milanzi na aliyekuwa Diwani wa Sinza, Salim Mwaking’ida imeahirishwa baada ya upande wa mashitaka kuomba kesi iahirishwe kwa sababu hawajamaliza maandalizi ya maelezo hayo.

Wakili wa Serikali, Awamu Mbangwa alitoa ombi hilo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mgeta ambaye alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 17 mwaka huu vigogo hao wasomewe maelezo ya awali.

Simba, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Malinzi wanadaiwa Septemba 2, 2009 Dar es Salaam, walikula njama ya kuchepusha fedha kinyume na kifungu cha 29 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 11 ya 2007.

Aidha wanadaiwa katika shitaka jingine kuwa Septemba 2, 2009 Dar es Salaam walighushi barua wakionesha kuwepo kwa kiwango zaidi cha fedha kwenye akaunti zote za benki za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) Ltd wakati wakijua kuwa si kweli.

Septemba 2, 2009 Simba akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya UDA na Malinzi akiwa Meneja Mkuu wa UDA, kwa pamoja wanadaiwa walichepusha Sh milioni 320 wakijifanya ni maalipo ya awali ya mauzo ya hisa katika shirika hilo fedha ambazo walijipatia kutokana na nyadhifa zao.

Kati ya Septemba 3, 2009 na Machi 31, 2010 jijini Dar es Salaam, Simba na Milanzi wanadaiwa walijipatia Sh milioni 320 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa Robert Kisena wakijifanya ni sehemu ya malipo ya hisa za shirika hilo la UDA.

Aidha Septemba 3, 2009 na Machi 31, 2010 jijini Dar es Salaam, Simba na Milanzi kwa nyadhifa zao wanadaiwa walichepusha Sh milioni 320 wakijifanya ni malipo ya awali ya ununuzi wa hisa katika UDA na kulisababishia shirika hilo madhara kwa kupata hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Washtakiwa hao wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 9 na Februari 11, 2011 jijini Dar es Salaam, wakitekeleza majukumu yao, kwa makusudi walitumia vibaya madaraka yao kwa kugawa hisa 7,880,330 zisizotumika za UDA kitendo ambacho ni uvunjwaji wa masharti ya vifungu vya ushirikiano katika kampuni.

Mwendesha mashtaka huyo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), alidai kuwa Februari 11,2011 jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao wakiwa waajiriwa wa UDA, walishindwa kuchukua tahadhari zinazostahili na kumuuzia Simon hisa 7,880,303 zisizotumika za UDA kwa bei ya Sh bilioni 1. 14.

Wanadaiwa walifanya hivyo bila kufuata utaratibu wa zabuni ambao ungetoa nafasi kwa mnunuzi kutoa ofa ya bei inayolingana na thamani ya hisa hizo, jambo ambalo liliisababishia UDA hasara ya Sh bilioni 2.37.