Apinga ushindi wa Malocha jimbo la Kwela

ALIYEKUWA mgombea ubunge Jimbo la Kwela mkoani Rukwa kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Daniel Nafthal Ngogo, jana alfajiri alitoka nje ya ukumbi akibubujikwa na machozi huku akipinga matokeo yalioonyesha kwamba ameshindwa.

Ngogo, kijana mwenye umri wa miaka 26 na msomi wa chuo kikuu alijikuta akibubujikwa machozi na kutoka nje akisindikizwa na mawakala wake baada ya Msimamizi wa Uchaguzi, Adam Missana kusema anaendelea kutangaza matokeo baada ya mgombea huyo kukataa kutia saini akitaka kata moja irudie uchaguzi.

Kabla ya kuondoka kwenye ukumbi akimwaga machozi, Ngogo alitaka masanduku ya kura yasifunguliwe ili kuthibitisha madai yao kuwa matokeo yamechakachuliwa. Ngogo pia alikuwa akidai kwamba masanduku ya kura yalikaa kwenye ofisi ya msimamizi wa uchaguzi kwa muda mrefu bila kuwa na ulinzi wa wasimamizi wao, hali ambayo ilimpa wasiwasi kama matokeo yanayotangazwa ni sahihi au yamechachakachuliwa.

Matokeo ya ubunge wa jimbo hilo lenye kata 26, yalibidi kusubiri matokeo ya kata moja ya Milepa ambayo ilichelewa kufanya uchaguzi kutokana na watu kuvamia gari lililokuwa linapeleka vifaa vya uchaguzi katika jimbo hilo na kuvichoma moto wakituhumu kuwa ni kura feki.

Msimamizi wa uchaguzi, hata hivyo alisema kisheria hana mamlaka ya kutoa aumuzi wa kata yoyote ile kurudia uchaguzi na hivyo akasema yeye ataendelea kutangaza matokeo. “Hata hivyo, mgombea unayo nafasi kupinga matokeo haya ya uchaguzi mahakamani,” alisema Missana.

Katika uchaguzi huo, Missana alimtangaza mgombea wa CCM aliyekuwa akitetea nafasi hiyo kwa mara nyingine, Ignas Malocha kuwa mshindi wa Jimbo la Kwela baada ya kupata kura 44,333 dhidi ya Ngogo aliyejipatia kura 39,615. Madaraka Maroub Hamis (ACT–Wazalendo ) aliambulia kura 968.