Mji Mkongwe Kilosa utajengwa upya kudhibiti mafuriko

JUMUIYA ya Nchi za Ulaya (EU) imetoa msaada wa Euro bilioni 5.1 kwa lengo la kusaidia kuujenga upya mji wa Kilosa na maeneo ya Mji Mkongwe katika wilaya hiyo. Miradi inayotekelezwa chini ya ufadhili wa EU ni ujenzi wa barabara za ndani, zahanati, shule mbili, mfumo wa maji safi na salama ya bomba na miundombinu ya usambazaji wa umeme maeneo ya mji mpya yanayojulikana kama Njia Panda, Kondoa na Kilimani.

EU imeamua kutoa fedha hizo ili kunusuru wilaya hiyo ulioharibiwa na mafuriko yaliyotokea vipindi vya miaka 2009/2010 na 2013/2014 katika kata 10 kati ya kata 35 za wilaya hiyo. Mafuriko hayo yameharibu miundombinu za kijamii na kiuchumi, makazi ya watu na mashamba ambapo zaidi ya wananchi 26,103 wa mji wa Kilosa wanahitaji msaada wa kibinadamu baada ya kuathiriwa na mafuriko hayo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa, Idd Mshili kwa kutambua madhara hayo EU imetoa kiasi cha fedha hizo kwa ajili ya kuijenga upya Kilosa ili kuondokana na tatizo la mafuriko. Mshili anasema, fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara, mifereji ya maji ya mvua, makalvati kwa maeneo ya uhindini na eneo la mji uliopo ng’ambo ya reli mjini Kilosa.

EU imetoa msaada wa Euro 5,178,241.36 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa zahanati, nyumba mbili za waganga na shule mbili za msingi, moja katika eneo la Kilimani yenye vyumba vya madarasa 10 ofisi ya walimu, maktaba pamoja na vyoo vya wanafunzi. Mshili anasema shule ya pili itajengwa eneo la njia panda yenye vyumba vya madarasa 12, nyumba mbili za walimu, maktaba, ofisi pamoja na vyoo vya wanafunzi.

Mradi wa kwanza utagharimu Euro 1,721,947. 12 bila kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ambazo ni sawa na Sh 4,097,909,947 na ujenzi wake unasimamiwa na Mhandisi mkazi, Godlisten Mawa kutoka Kampuni ya Rans ya Zanzibar. Mradi huo ulianza Januari 2014 na ulipangwa kumalizika mwishoni mwa Novemba mwaka huu. Hadi sasa kazi ambazo zimefanyika ni ujenzi wa ofisi, maktaba, madarasa 12 , nyumba mbili za walimu, matangi ya kuhifadhi maji ya mvua, ujenzi wa jengo la zahanati na nyumba ya mganga kwa gharama ya Euro 989,182.01 sawa na Sh 2,354,065,239.

Mshili anasema kiasi cha fedha zimetumika ni ambapo mradi umefikia kiwango cha asilimia 93 na hatua ya iliyobakia ni umaliziaji wa kupiga rangi na kufunga madirisha. Shule hizo mbili za kisasa zimejengwa kwenye miinuko ili kuwawezesha wanafunzi wa shule mbili tofauti zilizobomolewa baada ya kukumbwa na mafuriko makubwa ya mvua mwaka 2009/2010.

Mafuriko hayo yamewaathiri zaidi wakazi wa eneo la Behewa na Kata ya Mbumi na kuharibu miundombinu ya aina mbalimbali na pia yameathiri kwa kiwango kikubwa uharibifu wa shule tatu za Msingi ya Mkondoa, Mkwatani na Madaraka kubomoka. Hatua hiyo iliulazimu uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa, kuwahamishia wanafunzi wote wa shule hizo kwenda kuendelea na masomo ya katika shule zingine za Mazinyungu, Kilosa Town na Manzese.

“Ujenzi wa shule ya Njia Panda, walengwa wake ni wanafunzi waliokuwa wakisoma shule zilizopata maafa ya mafuriko mwaka 2009/2010 ambao kwa sasa wamechanganywa kwenye shule nyingine,” anasema Mshili. Ingawa mradi wa zahanati ulitarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, matumizi ya zahanati hiyo huenda yakachelewa kidogo kutokana na changamoto za upatikanaji wa samani, vifaa tiba na rasilimali watu.

Mradi mwingine ni wa barabara za Njia Panda na Kilimani unaojengwa kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilometa na ukarabati wa barabara za mkoa zenye urefu wa kilometa 2.5 wilayani humo kwa gharama ya Euro 1,996,325:50 sawa na Sh 4,750,875,388. Anasema mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Nandhra chini ya usimamizi wa Meneja mradi, Prenidas Guptan ambapo kiwango cha kazi kimefikia asilimia 50.

Pia anasema kampuni hiyo inakarabati barabara za mjini Kilosa na Uhindini zenye urefu wa kilometa kumi kwa kiwango cha changarawe kwa gharama za Euro 625,726. 32 sawa na Sh 1,489,109,754 na tayari mkandarasi ameshalipwa Euro 431,341.17. “Manufaa ya mradi huu wa ukarabati wa barabara ambazo zimeharibiwa na mafuriko zitawanufaisha zaidi ya wakazi 10,000 kwa kukingwa na mafuriko,” Mshili anasema.

Kwa upande wa Halmashauri tumepanga kuweka lami barabara zenye urefu wa kilometa tano kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017. Mshili anasema fedha zilizotolewa na EU zinatumika pia kwa mradi wa usambazaji wa umeme eneo la Njia Panda na Kilimani, na umetumia Euro 270,870 na kazi hiyo imekamilika kwa asilimia 100. Katika upatikanaji wa huduma bora za maji safi na salama kwa mji mpya wa Kilosa, EU imesaidia ujenzi wa mradi wa maji na kutumia Euro 563,372.42 ambapo matangi matatu yenye uwezo wa ujazo wa lita 50,000 kila moja yamejengwa.

Mshili anasema mradi huo umekamilika kwa kujengwa visima vitatu na kuwekwa mtandao wa maji wenye urefu wa kilometa 18 na ujenzi wa vituo 30 umefanyika ambao utahudumia kaya zenye watu 7,500. Mkuu wa wilaya ya Kilosa, John Henjewele, anasema kutokana na kuboreshwa kwa mji wa Kilosa, halmashauri ya wilaya itakuwa na jukumu la kutunga sheria ndogo za kusimamia suala la usafi wa mazingira na mipango thabiti ya mji wa Kilosa.

“Mji wa Kilosa sasa ni tofauti na ulivyokuwepo miaka ya nyuma, ni mji mkongwe lakini sasa umeboreshwa kwa kuwekewa huduma zote muhimu eneo la mji mpya,“ anasema Henjewele. Mkuu huyo wa wilaya anaishukuru Jumuiya ya Nchi za Ulaya kwa kuwajali wananchi wa wilaya ya Kilosa na Watanzania kwa ujumla kwa kutoa fedha hizo ambazo zinatumika kuendeleza mji wa Kilosa uwe wa kisasa na wenye mandhari za kuwavutia wageni na wenyeji wa wilaya ya Kilosa.

Henjewele ameutaka uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kusimamia kwa karibu masuala ya mipango miji ili kuepusha kila mmoja kujenga anavyo taka. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa mji wa Kilosa Jumuiya ya EU kwa kutoa fedha ambazo zimefanikisha kujengwa kwa mji mpya wa kisasa utakaokuwa ni kivutuo cha wageni na wakazi wa wilaya ya Kilosa.

Mkazi wa Masense C katika mji wa Kilosa, Tatu Hussein, anasema kuwa licha ya kujengwa kwa mji mpya wa kisasa, kuboreshwa kwa huduma ya maji katika mji huo kwa msaada wa EU kumewaondolea kero ya maji waliokuwa wakiipata siku za nyuma. Mjini Kilosa, anaelezea kuwa mafuriko yaliyotokea mwaka 2009/2010 yanafananishwa na yale yaliyotokea mwaka 1964.

Walieleza kuwa mafuriko katika bonde la mto Mkondoa yalianza kujitokeza mwaka 1940 wakati wa utawala wa ukoloni wa Kijerumani ambao uliamua kukabiliana na tatizo hilo mwaka 1948 kwa kujenga kingo za mto Mkondoa na kupanda miti na majani aina mbalimbali kando kando ya mto huo.

Mafuriko mengine yaliukumba mji wa Kilosa ni ya mwaka 1997/1978 wakati wa mvua kubwa za el-nino, ambazo ziliharibu miundombinu ya mto Mkondoa na kuvunja kingo za mto huo na kusababisha madhara kwa wananchi. Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kilosa, mafuriko ya Desemba mwaka 2009 yameharibu tena kingo za Mto Mkondoa unaokatisha katika mji wa Kilosa kufurika maji ya mvua na kumwaga maji katika makazi ya watu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mafuriko ya Desemba 2009, yaendelea hadi Januari 5 mwaka 2010 kusababisha vifo vya watu wawili kuathiri watu 23,980 sawa na kaya 5, 605. Katika mafuriko hayo nyumba 4,699 zilizingirwa na maji na nyingine 1,143 kubomoka, ambapo kambi 16 za muda zilianzishwa na kuwahifadhi waathirika wapatao 9,970. Kutokana na idadi kubwa ya waathirika, kambi nyingi zilijengwa kwa ajili ya kuwahifadhi waathirika ikiwemo ya Kondoa kwa wakati huo ilikuwa na kaya 291 sawa na watu 948 , kambi nyingine ya muda ilijengwa eneo la Kimamba na kuhifadhi kaya 230.

Licha ya kuanzishwa kwa kambi ndogo za muda kwenye maeneo hayo pia ilijengwa kambi kubwa eneo la Mazulia ikiwa na zaidi ya watu 6,700. Hivyo kutokana na madhara yaliyojitokeza nyakati hizo, baadhi ya mashirika mbalimbali ya ndani na nje yakiwemo ya kimataifa yalijitokeza kutoa misaada ya dharura ya kiutu na kifedha ikiwemo EU.