Katiba mpya ibane wabunge kuishi majimboni
- Imeandikwa tarehe 11 Septemba 2012
- By Sifa Lubasi, Dodoma
- Imesomwa mara: 452
SUALA la wabunge kuishi kwenye majimbo yao na uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya kwa kuzingatia maeneo waliyozaliwa ni baadhi ya mambo yaliyoibuliwa katika mjadala wa katiba uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Hombolo.
Mmoja wa wachangiaji ambaye alijitambulisha kama mwenyekiti wa kijiji cha Hombolo, Jared Mtawa alisema kitendo cha wabunge kutelekeza majimbo yao na kuishi Dar es Salaam kunasababisha kero za wananchi zisifike kunakotakiwa.
Aidha walisema kuteuliwa kwa wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka mahali walipozaliwa kutaongeza ufanisi wa kazi kwani ni wazawa wanafahamu vizuri maeneo waliyozaliwa tofauti na kumpa mtu ukuu wa Mkoa ambao hafahamu mazingira yake.
Akitoa maoni yake wakati wa mjadala wa katiba uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo Mjini Dodoma ulioandaliwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Dodoma Mjini (DUNGONET), alisema pia haja ya kuwa na Serikali moja ili kuboresha utendaji na kuondoa migogoro ya muungano kati ya Tanzania bara na Zanzibar
Akizungumzia juu ya suala la ukubwa wa Serikali alishauri kuwe na baraza dogo la Mawaziri.
“Pia katiba itamke ni mwiko wanaume kuvaa milegezo na wanawake kuvaa nguo fupi zinazodhalilisha jamii au zile zilizo kifua wazi na pia ioneshe kuwa ndoa iwe kwa watu wa jinsia tofauti na si kwa jinsia moja tu,” alisema.
Mwananchi mwingine Christopher Chawaba alisema kuwa, Katiba mpya izungumzie suala la kuboresha maslahi ya walimu ili kusiwe na migomo, hali ambayo itasaidia hata kuboresha ufundishaji mashuleni.
Mchungaji Samweli Chilewa wa kijiji cha Ipala alisema kuwa Katiba mpya impe kila mwananchi haki ya kumiliki ardhi.
Pia uteuzi wa wakuu wa idara mbalimbali uzingatie taaluma na si vinginevyo. Awali, wakili wa kijitegemea Elias Machibya alisema kuwa, Katiba ijayo ni muhimu ikaeleza wajibu wa vyama vya siasa.
Alisema kuwa Tanzania inajadili Katiba wakati Zanzibar ikiwa imeshafikia maamuzi ya katiba yao. Wachangiaji wengine walitaka Tume ya Katiba kuwa makini kwa lengo la kuhakikisha kuwa wajanja hawapenyi kwenye mchakato wa kukusanya maoni ili ipatikane katiba iliyotokana na mawazo ya wananchi na si vinginevyo.
Wakitoa maoni yao baadhi ya washiriki walitaka tume hiyo kuwa makini ili maoni yanayotolewa na wananchi yaingizwe kwenye katiba na si kuchukua mawazo ya watu wachache ambao wanataka maslahi zaidi.


