Uwezeshaji kaya masikini Sikonge waenda vyema

KAYA masikini 4,299 katika wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, zimenufaika na fedha za mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Awamu ya Tatu wenye dhamira ya kunusuru kaya masikini baada ya kuwezeshwa kiasi cha Sh 194,240.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Shadrack Mhagama alisema lengo la kuwezesha kaya masikini kupitia Mpango wa Tasaf Awamu ya Tatu limefikiwa ambapo kaya masikini zipatazo 4,299 kati ya kaya 4,310 tayari zimenufaika na mradi huo.

Mhagama alisema zoezi la uhawilishaji fedha kwa ajili ya kaya hizo limefanyika vizuri na kwa malipo ya kwanza fedha taslimu Sh 194,240,000 zimelipwa kwa walengwa kaya 4,299 kati ya 4,310 zilizoandikishwa, kaya 11 hazikulipwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufariki wahusika, kuhama eneo husika (wafugaji) na wengine kutohudhuria siku ya malipo na jumla ya Sh 472,000 hazikutumika.

Aliongeza kuwa katika malipo ya pili, kaya 4,129 kati ya 4,310 zililipwa na kaya 181 hazikulipwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufariki wahusika, kutohudhuria siku ya malipo na baadhi ya wahusika kufukuzwa katika eneo la hifadhi la Nyahua walilokuwa wakiishi kinyume cha taratibu, fedha zilizotumika ni Sh 170,860,000 na ambazo hazikutumika ni Sh 7,504,000.

“Uwezeshaji kaya masikini umeenda vizuri kwa walengwa wote waliotambuliwa katika wilaya nzima ya Sikonge licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza na kufanya baadhi yao washindwe kupata uwezeshaji huo,” aliongeza.

Aidha, alibainisha kuwa dhamira ya serikali ni kunusuru kaya masikini zote hapa nchini kwa kuziwezesha kiuchumi ili kuondokana na umasikini walio nao huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa waratibu wa Tasaf ili wasipitwe na fursa hiyo adimu.

Mratibu wa Tasaf wilayani Sikonge, Claud Nkanwa alitoa takwimu za jumla ya kaya masikini zilizotambuliwa awali na zilizohakikiwa na kuandikishwa kwa ajili ya kuwezeshwa katika kila kata, vijiji na vitongoji vyake vyote kuwa ni kata zote 17 za wilaya hiyo, vijiji 46 na vitongoji 189.

Alitaja takwimu za waliotambuliwa kwa kila kata huku walioandikishwa wakiwa kwenye mabano kuwa ni Chabutwa 412 (352), Igigwa 701 (636), Ipole 250 (192), Sikonge 269 (242), Tutuo 431 (354), Misheni 190 (145), Mole 445 (425), Kiloleli 198 (171), Kipanga 150 (129), Mpombwe 131 (120), Pangale 228 (193), Usunga 212 (199), Kipili 596 (463), Kiloli 229 (190), Kitunda 223 (200), Ngoywa 153 (148) na Kisanga 144 (136).