Wakulima kukopeshwa pembejeo
- Imeandikwa tarehe 13 Septemba 2012
- By Veronica Mheta, Arusha
- Imesomwa mara: 350
SERIKALI inatarajia kuendesha mfumo mpya wa utoaji ruzuku za pembejeo za kilimo kwa mkopo kuanzia mwakani ili kuwanufaisha wakulima wengi zaidi.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama ametoa taarifa hiyo leo wakati alipokuwa akifungua mkutano wa kutathmini mfumo wa zamani na kuelezea mfumo mpya wa vocha.
Alisema uamuzi huo wa Serikali unatokana na kugundua changamoto katika mfumo wa zamani wa mwaka 2008/2009 uliogubikwa na malalamiko ya wizi wa pembejeo na waliopewa dhamana ya kusambaza walikiuka makubaliano na Serikali.
Gama alisema katika mfumo wa awali makundi ya wanasiasa, wataalamu na watu mbalimbali walilalamikia mawakala wa pembejeo kwamba wamekuwa wakijinufaisha wenyewe .
Alisema katika maeneo mengine walisaini vocha bila kufikisha pembejeo hizo.
“Hapa unaona wakala anasaini vocha, lakini hakuna anachopeleka kwa wakulima, au anapeleka mbegu mbovu huku wakati msimu wa kilimo umekwisha na matokeo yake hasara kwa wakulima,”alisema Gama.
Aliongeza kuwa mfumo huo utahusisha vyama vya ushirika vya wakulima vijijini pamoja na vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) ambavyo kabla ya kukabidhiwa ruzuku, watapatiwa elimu kuhusu mfumo huo, ili uwe na tija kwa wakulima na Serikali kwa ujumla.
Alishauri Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuendesha mafunzo maalumu kwa wakulima ili kuwaondoa woga pamoja kwa kuwaelimisha kuhusu mfumo huo mpya hususan namna ya upatikanaji wa mikopo hiyo na kuirejesha.
Mkurugenzi Msaidizi wa pembejeo za kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Dk Mshindo Msolla alisema mkutano huo una umuhimu mkubwa kwa wadau hao kwakuwa unalenga kuondoa uchakachuaji wa pembejeo na malalamiko yaliyokuwepo.
Alisema mabadiliko matatu yatakayokuwemo katika mfumo huo mpya, ni mawakala wa pembejeo kuteuliwa na kampuni badala ya kamati za pembejeo za wilaya kama ilivyozoeleka.
Alisema katika mfumo huo wakala atawakilisha kampuni zaidi ya moja na wakala zaidi ya mmoja atafanya kazi katika vijiji mbalimbali, ili kuongeza ushindani kuepuka kasoro zilizokuwa zikijitokeza ikiwemo usambazaji wa pembejeo zisizo na ubora na wizi.


