21Mei2013

 

TBA kujenga nyumba za watumishi 2,500

WAKALA wa Majengo nchini (TBA) unatarajia kujenga nyumba 2,500 kwa ajili ya kutumiwa na watumishi wa umma wa nchini.

Hayo yalisemwa jana wilayani Ukerewe na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo nchini, Elius Mwakalinga alipokuwa akitoa taarifa ya ujenzi wa nyumba mbili za watumishi wa umma mjini Nansio kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika hafla ya kuweka jiwe la msingi katika nyumba hizo.

Mwakalinga alisema hatua ya ujenzi wa nyumba hizo za watumishi inaendana na dira ya Taifa ya 2025, utekelezaji wa Mpango mkakati, Mkurabita pamoja na malengo ya milenia.

“Ujenzi wa nyumba hizi ni mwanzo wa utekelezaji wa mpango wa Serikali, kwani baada ya hatua hii, katika mwaka huu wa fedha Wakala wa Majengo utajikita katika kujenga nyumba 2,500 kwa ajili ya watumishi wa umma wote nchini”, alisema na kuongeza kuwa nyumba hizo mbili zimejengwa kwa gharama ya Sh milioni 160.

Alisema ujenzi wa nyumba zitakazojengwa na hizo zilizowekewa mawe ya msingi na Waziri Mkuu umezingatia pamoja na mambo mengine, ujenzi wa kitaalamu na wa kisasa na zitakuwa imara kwa ajili ya kutumiwa na watumishi wa umma.

“Nyumba za leo zimejengwa kwa kufuata ramani ya aina moja, ambayo hata kwa zile zitakazojengwa ni ile iliyosanifiwa na Wakala wa Majengo kwa kulenga kada ya kati ya watumishi wa umma”, alisema na kuongeza kuwa nyumba za aina hiyo zilikwishajengwa katika maeneo ya Mbweni jijini Dar es Salaam, Pasiansi jijini Mwanza na eneo la Cheyo katika Manispaa ya Tabora, mkoani Tabora.