Msekwa kuiuzia Serikali nyumba
- Imeandikwa tarehe 13 Septemba 2012
- By Nashon Kennedy, Ukerewe
- Imesomwa mara: 808
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa anatarajia kuiuzia Serikali ya Wilaya ya Ukerewe nyumba yake iliyo katika eneo la Bomani mjini Nansio ambayo imekuwa ikitumiwa na viongozi wa ngazi ya kitaifa wanaokwenda wilayani humo kwa ziara za kikazi.
Uamuzi wa Msekwa kuuza nyumba yake hiyo umetangazwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mary Tesha alipokuwa akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye anaendelea na ziara yake ya siku saba mkoani Mwanza.
Tesha alisema wilaya imefikia uamuzi wa kununua nyumba hiyo ya Msekwa kutokana na wilaya kutokuwa na nyumba ya kupumzikia viongozi wakuu wa Serikali.
“Kutokana na hali hiyo wilaya imebainisha nyumba mbili, ambazo zinafaa kuwa nyumba ya kupumzikia, nazo ni ya Msekwa ambayo mara nyingi viongozi wakuu wa kiserikali wamekuwa wakiitumia kila wanapotembelea wilaya yetu na nyumba ya pili ni ya Masumbuko Mtani”, alisema Tesha.
Tesha alisema katika ziara yake mwaka 2010 wilayani Ukerewe, Rais Jakaya Kikwete aliagiza nyumba chakavu ya Mkuu wa Wilaya iingizwe kwenye bajeti ya mkoa ya mwaka 2012/13 ili iweze kujengwa nyumba mpya na ya kisasa.
“Lakini kwa bahati mbaya bajeti ya maendeleo ya mkoa kwa mwaka huu wa fedha imepungua sana na hivyo nyumba hiyo ya Mkuu wa Wilaya haikuweza kuingizwa kwenye bajeti kwa ajili ya kujengwa”, alisema Tesha.
Alisema kwa upande wa nyumba ya kupumzikia viongozi wakuu wa kitaifa Rais aliagiza wilaya ianze kubainisha nyumba inayofaa ikiwemo nyumba hiyo ya kupumzikia viongozi ya Pius Msekwa.
“Wilaya imeona eneo hili pamoja na nyumba ya Sumbuko Chipanda zinafaa kukaguliwa na mojawapo kununuliwa kuwa nyumba ya kupumzikia wageni, ama zote mbili zinunuliwe na moja iwe ya Mkuu wa Wilaya na eneo la nyumba ya Mkuu wa Wilaya litumike kujengwa nyumba za maofisa wakuu wa Serikali Kuu”, alisema Tesha.
Waziri Mkuu aliweza kuzitembelea nyumba hizo na kuafikiana na mapendekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya kuzinunua.


