Serikali, wanaharakati kuongeza kasi vita ya unyanyasaji kijinsia

SERIKALI wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro imesema itasaidiana na wanaharakati wilayani na mkoani humo kuhakikisha takwimu za watoto wenye ulemavu zinapatikana kwa haraka ili wapate huduma zinazostahili.

Hakikisho hili limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga, wakati wa uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Kanda ya Kaskazini, uliofanyika mjini Moshi, jana.

“Inasikitisha kusikia kupitia taarifa yenu kuwa upatikanaji wa takwimu hizi ni changamoto kwa vile wanafichwa, huku ni kuwanyanyasa watoto wa aina hii kisaikolojia na ukatili kwa watoto,” alisema.

Alitoa rai kwa wanaharakati kupitia kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo, kufanya utaratibu wa kushirikiana na Uongozi wa Shule ya Polisi Tanzania (TPS), ili kubadilishana uzoefu na kuimarisha vita dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi hayo, Honoratha Nasua, alisema moja ya changamoto wanazokutana nazo ni upatikanaji wa takwimu za watoto wenye ulemavu ambao wanahitaji msaada mkubwa.

Hata hivyo, alisema wanaharakati wameamua kuvalia njuga suala hilo kupitia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ya “Funguka, mlinde mtoto apate elimu”, kuhakikisha idadi yao inapatikana na wanapata huduma zinastahili.

Akielezea changamoto nyingine wanazokabiliana nazo, Honoratha alisema ni pamoja na ile ya watuhumiwa wa ukeketaji kuhamishia ukatili huo kwa watoto wachanga. Honoratha, ambaye pia ni Meneja Programu wa Asasi Inayopinga Ukeketaji (NAFGEM), alitoa mwito kwa wadau mbalimbali kutoa ushirikiano wao wa dhati kutokana na ukeketaji kuwafanya waathirika kuona wameshakuwa watu wazima na kuacha shule ili waolewe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linashughulika na haki za Binadamu na jinsia la Kwieco, Elizabeth Minde, alitoa rai kwa wazazi kujenga tabia ya kuwlainda watoto kwa saa 24, ili kuwaepusha vitendo vya ukatili dhidi yao.