‘Elimisheni wanamgambo waache unyanyasaji’

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umezitaka Halmashauri za Wilaya, Manispaa, Miji na Majiji nchini kujipanga na kuwaelimisha wanamgambo waache mara moja tabia ya kuwanyanyasa wajasiriamali wakiwemo wamachinga na mamalishe.

Ilisema haifurahishwi wala kuridhishwa na tabia za manyanyaso, uonevu na udhalilishaji unaokiuka misingi ya utu na heshima unaofanywa na baadhi ya wanangambo kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka ametoa msimamo huo jana wakati alipokutana na vijana wajasiriamali wa mkoa wa Dar es Salaam waliofika kuelezea changamoto mbali mbali wanazokabiliana.

Shaka alisema matumizi ya nguvu, ubabe kwa machinga na mama lishe kunyang’anywa bidhaa zao kukimbizwa wakati wakiwa kwenye shughuli halali za kujitafutia kipato sio jambo zuri.

“Serikali yetu iliianzisha kikosi cha mgambo kama askari wa akiba kwa lengo maalumu la kuimarisha ulinzi kwenye vijiji, vitongoji na mitaa, mgambo hawajaambiwa wapige watu, wapore bidhaa, masufuria ya wali na ugali au kumwaga nguo za machinga,” alieleza Shaka.

Aidha, alisema UVCCM itamuandikia barua rasmi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili kumfahamisha kuwa umoja huo hauridhishwi na vitendo hivyo vya uonevu na ukandamizaji. Kaimu Katibu mkuu huyo alisema mgambo ni kikosi chenye nidhamu, kuheshimu miiko na maadili lakini pia baadhi ya askari kikosi hicho walikwenda mstari wa mbele vitani kupambana na majeshi ya uvamizi ya Uganda katika vita ya Kagera mwaka 1978 /1979.

Alisema UVCCM wanakiheshimu na kukiamini na kukitegemea kikosi hicho ila baadhi ya askari wake sasa wamegeuka kuwa sehemu ya kero huku wakiigombanisha serikali na watu wake kwa vitendo vyao vya piga piga wafanyabiashara wadogo.

“Halmashauri zetu, manispaa, miji na majiji wakijipanga, kuweka mazingira bora na rafiki kati yao na wafanyabiashara wakubwa na wadogo, mambo yatakwenda vizuri bila kuharibika na kuvutana,” alisisitiza shaka.

Hata hivyo, aliwataka machinga, bodaboda na mamalishe kuheshimu sheria, kutunza mazingira kwa kufanya usafi sambamba na makundi yao kujenga umoja wa wafanyabiashara ili kujisajili kisheria hatimaye waweze kupata mikopo kwenye taasisi za fedha.