Vituo vya afya 286 havina maji Dodoma

VITUO 286 kati ya vituo vya afya 402 vilivyopo mkoani Dodoma havina maji kabisa na hivyo kuleta shida kubwa ya usafi binafsi kwa wanaofika kupata huduma katika vituo hivyo.

Aidha vituo vyenyewe vinakuwa na kazi ya ziada kuvifanya kuwa visafi. Kutokana na mazingira hayo wahudumu katika vituo vya afya mkoani Dodoma hulazimika kuchota maji nje ya vituo hivyo ili kuwahudumia wagonjwa wanaofika kupatiwa matibabu.

Hayo yalibainishwa jana na waganga wa wilaya za Chamwino na Mpwapwa Mkoani hapa kwenye kikao cha bodi ya washauri wa mradi wa Maji kwa afya ya Jamii (Mkaji) kilichokuwa na lengo la kujadili mafanikio, changamoto na jinsi ya kuzitatua.

Katika kikao hicho Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk Said Mawji alisema hali ya upatikanaji wa maji kwenye vituo vya afya wilayani mwake siyo ya kuridhisha kwani wauguzi hulazimika kwenda kutafuta maji nje ya vituo kwa ajili ya matumizi ya wagonjwa.

Alisema vituo vingi vya afya na zahanati vinakabiliwa na ukosefu wa maji kutokana na jiografia ya eneo vilipo kuwa na milima na hata maji yanayopatikana kuwa si safi na salama. Mganga huyo pia alibainisha kuwa mradi wa Mkaji ambao unahusisha pia ukarabati na utengenezaji wa miundombinu ya maji katika vituo vya kutolea huduma za afya ni moja ya mradi muhimu na kuitaka serikali kuunga mkono suala hilo.

Ofisa Afya wa wilaya ya Chamwino, Dk Cathbert Kongola alisema hali ya upatikanaji wa maji katika vituo vya afya ni asilimia 50 tu. Alisema miundombinu ya maji haijafika kwenye vituo hali ambayo huwalazimu wananchi kubeba maji wapokwenda kwenda vituo kupata huduma za matibabu.

Ofisa Mradi wa Mkaji, Sostenes Gabriel alisema mradi huo una mpango wa kuvifikia jumla ya vituo vya afya na zahanati 100 katika wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma ambapo katika kila wilaya watachagua baadhi ya vituo.