Wafanyakazi taasisi za fedha walia na waajiri
- Imeandikwa tarehe 14 Septemba 2012
- By Oscar Job
- Imesomwa mara: 225
CHAMA cha wafanyakazi kinachoundwa na taasisi za Kifedha, Viwanda, Benki, Biashara na Mazao ya Kilimo (FIBUCA) kimelalamikia vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na baadhi ya waajiri na kuitaka Serikali kuvunja ukimya juu ya suala hilo.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni Dar es Salaam na Rais wa Fibuca, Joseph Massana wakati wa mkutano wa Kamati ya utendaji wa Chama hicho ambapo mbali na suala hilo pia alimuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) kuchunguza utaratibu wa malipo ya mishahara kwa wafanyakazi wa taasisi mbalimbali hususan benki.
Kwa mujibu wa Massana, kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya ukiukwaji wa haki za wafanyakazi katika taasisi mbalimbali, jambo alilodai kuwa kimsingi linapaswa kupigiwa kelele ili kulinda haki za wafanyakazi hao.
“Katika mfumo wa sasa uhalifu dhidi ya haki za wafanyakazi ni mkubwa, mfumo huu umeharibu utendaji kwa kusababisha kuwapo matabaka mbalimbali kwa wafanyakazi ambayo katika utaratibu wa kawaida ni makosa kwa kuwa yanawanyima haki walio wengi na manufaa kwa walio wachache,” alisema Massana.
Huku akitolea mfano wa baadhi ya taasisi zinazoonesha ukiukwaji wa haki hizo, Rais huyo alisema umefika wakati muafaka kwa Chama hicho kuchukua hatua stahiki za waajiri wote wenye tabia kama hizo ili kuwa fundisho kwao wakati huu aliodai kuwa kila mtu ana wajibu wa kula matunda ya kazi yake.
Alisema katika uchunguzi waliofanya, wamebaini kuwapo kwa utaratibu wa aina mbili wa malipo ya mishahara kwa wafanyakazi hususani katika taasisi za benki, jambo alilosema kuwa umefika wakati kwa (CAG) kufanya uchunguzi ili kubaini kasoro hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Cosmas Msigwa alikitaka chama hicho kuwasilisha malalamiko ya vitendo vyote wanavyoona havimtendei haki mfanyakazi ili viweze kufanyiwa kazi na kwamba kazi ya tume hiyo ni kushughulikia masuala hayo.
Kwa mujibu wa Msigwa, wafanyakazi wanapaswa kufahamu wajibu na taratibu za utendaji wa kazi zao, kabla ya kuingia mikataba ya kazi na kwamba kinyume na hapo ni kukiuka utaratibu ambao mwisho wa siku husababisha kutokea kwa malalamiko mbalimbali.


