Karata muhimu kwa Kilimanjaro Stars leo

TIMU ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kili Stars’ leo inashuka kwenye dimba la Awassa nchini Ethiopia kuwakabili wenyeji Ethiopia ukiwa ni mchezo wa robo fainali wa kusakata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Chalenji, inayoendelea nchini humo.

Kili Stars ilimaliza michezo ya makundi ikiwa vinara wa kundi A, kwa kujikusanyia pointi saba, huku Ethiopia wakiingia wakiwa nafasi ya tatu, baada ya kupata sare kwenye mchezo wa mwisho wa makundi na kufikisha pointi nne zilizowavusha hatua hiyo.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa mgumu na wenye ushindani mkali kutokana na wenyeji Ethiopia kutokubali kurudia makosa waliyoyafanya kwenye hatua ya makundi na kuwekwa katika wakati mgumu.

Ethiopia iliweza kushinda mchezo mmoja tu katika hatua ya makundi kwa kuifunga Somali mabao 2-0, huku ikifungwa bao 1-0 na Rwanda kwenye mchezo wa ufunguzi na kuonesha kiwango cha kawaida ambacho hakikuwa tishio kwa timu pinzani.

Kocha wa Ethiopia, Yohannes Sahle alisema mchezo wa leo utakuwa mgumu lakini watatumia uwenyeji wao kuweza kuifunga Kili Stars, ambayo imeonesha kufanya vizuri tangu kuanza kwa michuano hiyo.

Sahle alisema ameweza kuwasoma vizuri Kili Stars, katika mchezo wao wa Jumamosi hivyo hadhani kama atakuwa na kazi kubwa kuivusha Ethiopia kwenye nusu fainali na hatimaye fainali na kubakiza taji hilo nyumbani.

“Tumeanza kwa presha na kibaya zaidi tunacheza nyumbani mbele ya mashabiki wetu, lakini kitu kizuri ni kwamba nimezungumza na wachezaji baada ya mechi ya Jumamosi na kuelekezana mapungufu waliyokuwa nayo wapinzani wetu kila mmoja ameahidi kujituma na kupata ushindi,”alisema Sahle.

Kwa upande wake kocha wa Kili Stars, Abdallah Kibaden alisema hana presha na mchezo wa leo kwa sababu amewasoma vizuri wapinzani wao na ana uhakika kikosi chake kitavuka mtihani huo na kutinga hatua inayofuata.

Kibadeni alisema katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Ethiopia, aliwataka wachezaji wake kucheza bila ya presha kwa sababu walishatinga robo fainali na ndiyo maana akawapumzisha baadhi ya wachezaji wake nyota kwa ajili ya kuweka nguvu kwa pambano hilo.

“Hatuna presha tumejizatiti kuhakikisha tunawafunga na kuwatoa wenyeji kwa sababu nimewaona wakicheza na wana mapungufu mengi kwa kweli sidhani kama tuna sababu ya kushindwa kuwafunga,”alisema Kibadeni.

Mchezo huo utatanguliwa na robo fainali ya kwanza itakayozikutanisha Uganda na Malawi na Kili Stars, inapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kutokana na udhaifu wa wenyeji wao Ethiopia ambao uenyeji umeonekana kuwabeba.