Kanisa lasaidia wanafunzi 100 waliounguliwa shuleni
- Imeandikwa tarehe 16 Septemba 2012
- By Christopher Maregesi, Bunda
- Imesomwa mara: 337
MISAADA mbalimbali imeanza kutolewa kwa wanafunzi 100 wa shule binafsi ya sekondari ya Ikizu ya wilayani hapa walioathiriwa na moto uliotokea wiki iliyopita ambapo jana Kanisa la Waadventista la Sabato Jimbo la Mara limetoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh mil. 3.7.
Msaada uliotolewa na kanisa hilo kupitia idara yake inayojishughulisha na huduma za kijamii ya ADRA ni fulana 175, suruali 94, mashati 82, jaketi 42, masweta 122 mablanketi 83 na matandiko 94.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe ambaye aliukabidhi kwa uongozi wa shule hiyo, Mwenyekiti wa kanisa hilo jimboni humo Mchungaji Daudi Makoye alisema kanisa limeguswa na tukio hilo na litafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa watoto hao wanarejeshewa.
Mchungaji Makoye ambaye kanisa lake ndilo linalomiliki shule hiyo aliwapongeza wanafunzi kwa utulivu waliouonesha kipindi chote cha tukio hilo na kuendelea na masomo kana kwamba hawajaathirika na janga hilo na kuwataka waendelee hivyohivyo hata baada ya masomo yao.


