Masaju ahimiza ‘Hapa Kazi Tu’ shuleni

SHULE, vyuo na taasisi za elimu zimetakiwa kutekeleza ipasavyo kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ili kuwatayarisha na kuwandaa watoto na vijana kufanya kazi za kujiajiri wao wenyewe au kuajiriwa wanapomaliza masomo yao.

Hayo yamesemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju. Alisema hayo wakati wa mahafali ya 15 ya Shule ya sekondari ya Feza jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Masaju alizitaka taasisi hizo, kuwaandaa vijana hao kwa maisha yao baada ya shule na katika utumishi nchini.

“Tuishi kwa kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya ‘Hapa Kazi Tu’”, alisema. Alisema Serikali imeelekeza kwamba kuanzia Januari 2016 elimu itolewe bure kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha nne, hivyo hakutakuwa na sababu ya watoto wa shule za msingi au watoto waliofalu na kupata nafasi ya kusoma elimu ya sekondari, kutokusoma.

“Ninashauri wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi hizi za Serikali kwa maslahi na maendeleo ya watoto wetu na nchi yetu kwa ujumla,” alisema.