Kesi ya Mwale yanguruma

KESI ya Wakili maarufu Jijini hapa, Medium Mwale na wenzake watatu, imeanza kuunguruma katika Mahakama Kuu Kanda Kuu ya Arusha. Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Fadhili Said Mdemu (39) ambaye ni Mrakibu wa Jeshi la Polisi, alidai katika Mahakama Kuu hiyo jana kuwa washtakiwa hao, walifanya jaribio la kuchepusha dola za Marekani milioni 17.2 za msaada za kupambana na malaria na Ukimwi.

Fedha hizo zilitolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Global Fund na waliziingiza katika akaunti yao ya East African and Malaria and HIV and Support Programme, iliyopo tawi la Meru katika Benki ya CRDB Arusha. Mdemu alidai hayo mbele ya Jaji Gadi Mjemas, anayesikiliza kesi hiyo. Alidai yeye ndiye mpelelezi wa kesi hiyo kutoka kitengo cha masuala ya uhalifu wa kifedha Jiji Dar es Salaam na alipatiwa maelekezo na wakuu wake kazini Julai mwishoni 2011 kuwa aje Arusha kufuatilia akaunti hiyo ya CRDB tawi la Meru, kwani inataka kuchepusha fedha za msaada.

“Akaunti hii ina majina yanayofanana na akaunti ya Wizara ya Fedha na hivyo ilikuwa rahisi kwao kutaka kuchepusha fedha hizo kwa kughushi barua na kujifanya kama wao ndio Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ramadhani Khijjah, ambayo ilitoa maelekezo fedha hizo zisiingizwe akaunti ya wizara, badala yake iingizwe akaunti hiyo ya CRDB tawi la Meru Arusha, sababu ndio kwenye eneo la mradi wa Malaria na Ukimwi,”alidai.

Alidai mahakamani hapo kuwa baada ya barua hiyo kupelekwa Geneva, Uswisi, makao makuu ya Global Fund, wafadhili walielekeza fedha hizo ziingizwe katika akaunti hiyo ya Meru, lakini wakati fedha hizo zilipoelekezwa kuingizwa katika akaunti hiyo, Wizara ilipata taarifa za kuchepusha fedha hizo na kuanza kufuatilia. Alidai kuwa ndipo yeye (Mdemu) alikwenda Arusha katika tawi la CRDB Meru mkoani Arusha na kuonana na Meneja wa tawi hilo, Boniface Mwimbwa ambaye ni mmoja wa washitakiwa na kuomba taarifa za waliofungua akaunti hiyo; na hapo ndipo uchunguzi ulipoanza hadi kuwanasa watuhumiwa hao.

“Nilikuta signatory katika akaunti hiyo ya tawi la CRDB Meru Arusha ni Michael Crispen Chacha na mwenzake Anderson Marwa ambao walitambulishwa kisheria na Medium Mwale kupitia akaunti yake ya Mwale Advocate,” alidai. Baada ya shahidi kueleza sehemu ya ushahidi, Wakili upande wa mashtaka ambao ni serikali, Oswald Tibabyakyomya, aliomwonesha nyaraka za uchunguzi wake, kama anazifahamu ambazo ni pamoja na nakala za vitambulisho vya mkazi, taarifa benki na zingine, kisha kuomba mahakama ipokee kama kielelezo katika kesi hiyo.

Shahidi Mdemu alivipokea na kuihakikishia mahakama kuwa ni nyaraka anazozifahamu; na yeye ndio aliyehifadhi wakati anapeleleza kesi hiyo na kuomba mahakama ipokeee kama kielelezo. Mdemu alipomaliza kusema hivyo, Jaji aliamuru nyaraka zikaguliwe na upande wa utetezi, unaoongozwa na wakili Omary Omary akisaidiana na jopo la mawakili wenzake. Mawakili hao walikataa mahakama isipokee nyaraka hizo, kwa madai haziko sahihi na baadhi zimekosewa, kama vitambulisho vya makazi majina yapo mawili, lakini shahidi alitaja majina matatu na taarifa ya benki hazikuthibitishwa.

Pia walidai shahidi yeye ndio mpelelezi wa kesi hiyo na nyaraka hizo zake, hivyo hawaamini kama hajaghushi sababu zina mapungufu ya kisheria. Hali hiyo ilizua malumbano ya kisheria, huku Wakili Oswald Tibabyakyomya, akiomba mahakama izipokee kwa kuwa zimekidhi vigezo vyote vya kisheria. Baada ya malumbano ya zaidi ya saa tatu, Jaji Mjemas alisikiliza pande zote mbili na kuahirisha kesi hiyo hadi leo, atakapotoa maamuzi ya vielelezo, kama vipokelewe au la.

Kesi hiyo inawakabili Medium Mwale na wenzake Donbosco Gichana, Boniface Mwimbwa na Elias Ndejembi, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 42 tofauti tofauti, ikiwemo la utakatishaji fedha haramu, kughushi nyaraka na kukutwa na mali zilizopatikana kwa njia za uhalifu. Walisomewa mashtaka yao, kisha washtakiwa wote waliyakana.