DIMBWI LA MAHABA: Umuhimu wa zawadi katika uhusiano

ZAWADI ni moja ya chachandu au mbolea yenye nguvu katika uhusiano na jambo la msingi ni kuhakikisha zawadi husika inatolewa huku ikiwa imebeba ujumbe maalumu wa hisia zetu kwa wakati husika.

Tangu enzi za mababu zetu, zawadi imekuwa moja ya alama iliyokuwa ikitumiwa sana na wenza katika mchakato mzima wa kupalilia penzi na kudumisha uhusiano. Kuna baadhi ya watu wameshawahi kusikika wakidai kuwa zawadi ni kitu tu ambacho mtu hupewa na mara nyingi haina nafasi katika uhusiano, jambo ambalo si kweli.

Kama nilivyosema awali katika uhusiano, zawadi inaweza kuwa chachandu katika uhusiano, hasa zawadi hiyo ikitolewa kwa lengo maalumu, inaweza kujenga uhusiano husika na kuuimarisha zaidi. Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa zawadi unayotaka kutoa kwa mwenza wako, unaitoa wakati gani na kwa nini na kubwa zaidi ni zawadi gani.

Na hili ni muhimu kwa wanaume wanaotoa zawadi kwa mwanamke, kwa kuwa mara nyingi zawadi wanazopewa wanawake na hata wanaume, nyingi hubeba ujumbe wa hisia au tukio, jambo ambalo linatakiwa kupewa umakini kabla ya kutoa tu zawadi hiyo.

Chakuzingatia, hakikisha zawadi unayoichagua kumpatia mwenza wako iwe ya matumizi ya kwake mwenyewe, hivyo kama ni mwanamke unampatia mwenza wako zawadi, ni vyema kwanza uangalie aina ya maisha yake.

Kwa mfano zawadi ambazo wanawake wanaweza kupatia wenza wao, jambo la kwanza wanatakiwa watambue kuwa wanaume wengi wanapenda kuonekana watanashati na kunukia vizuri, ingawa kiukweli si wanaume wengi hasa wenye majukumu mengi wanaojali sana kuhusu muonekano wao.

Hivyo wanaume wa aina hiyo ni vyema kumchukulia zawadi kama vile manukato, deororants, vifaa vya kunyolea ndevu, mashati kuendana na suruali, tai na kama ni mvutaji wa sigara, hata kibiriti chenye muonekano mzuri pia kinaweza kuwa zawadi njema kwake.

Kwa wanawake pia ni rahisi kwani siku zote maua, kadi zenye maneno mazuri yanayoonyesha hisia zako, hereni, mkufu, bangili, khanga au vitenge, viatu hasa kuonesha unajua anavaa namba ngapi, manukato na vitu vidogo kama vile nguo za ndani, vinaweza kuujenga uhusiano wako.

Jambo la msingi katika kufanikisha uchaguzi wa zawadi ya mwenza wako ni kuhakikisha kuwa unatambua vitu ambavyo mwenza wako anapendelea, ili umpe na hivyo si tu itajenga uhusiano wenu, lakini pia itagusa moyo wake.

Usiogope kumpatia mwenza wako zawadi pale unapoona amekugusa katika uhusiano wako au pale unapoona anastahili zawadi hiyo, kwani huwezi jua, unaweza kujikuta uhusiano wako unachanua na kudumu kuliko ulivyotarajia kwa kitu kidogo tu kama zawadi.

Unapompatia mwenza wako zawadi, siku zote huonyesha kuwa unamjali, unampenda na kubwa zaidi unamthamini jambo ambalo linaweza kukusaidia hata kama uhusiano husika ulianza kulegalega.