Tumvumilie Mkwasa Stars

BAADHI ya wadau wa soka wameanza kuhoji uwezo wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 7-0 na Algeria. Mchezo huo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia ulifanyika zaidi ya wiki mbili zilizopita mjini Blida, Algeria.

Kutokana na matokeo hayo, Taifa Stars ilitolewa katika mbio za kuwania kufuzu Kombe la Dunia Kanda ya Afrika, baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam kutoka sare ya mabao 2-2.

Tunavyofahamu Taifa Stars inapofanya vibaya huwa hazikosi sababu ambazo si za kitaalamu na zaidi ni kutupiana lawama zisizo na msingi hasa kwa mashabiki, ambao wengi wao hujifanya makocha.

Kila mtu atasema lwake, kulingana na jinsi anavyoona inafaa, ikiwa ni kuhalalisha kipigo au kutaka kusukuma lawama kwa wengine kuhusiana na matokeo hayo mabovu. Hatutaki kuhoji kwa nini Stars imefungwa, lakini tunaweka tahadhari kwamba matokeo hayo yawe kichocheo cha kujipanga kwa ajili ya mechi zijazo za kimataifa.

Tukubali kwamba Algeria ipo juu katika soka, ndio maana hata hapa nyumbani tulitoka nao sare ya mabao 2-2, lakini wakaenda kutufunga kwao. Pia hata katika viwango vya ubora wa soka vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Algeria wapo nafasi ya 28 yaani wapo katika 30 bora, huku Tanzania ikiwa nafasi ya 132, yaani hata 100 bora hatupo.

Hata hivyo tunasema matokeo hayo yawe changamoto pia kwa Mkwasa kujiangalia na mikakati yake ya kuisuka Taifa Stars, maana tunahofu isijekuwa tunapiga hatua mbili mbele halafu tunarudi nane nyuma.

Ni wazi kwamba kocha huyu amekuwa akijitahidi kujenga timu kila mara na tunatambua juhudi zake, lakini hebu sasa atumie kipigo hicho kama ni changamoto katika kukisuka upya kikosi chake.

Tunajua kwamba kushinda na kushindwa ni sehemu ya mchezo na pia asiyekubali kushindwa si mshindani, lakini kuna kushindwa kwingine ni kwa kujitakia, hivyo hebu tujiulize hilo.