Mke wa kigogo Polisi atapeliwa
- Imeandikwa tarehe 20 Septemba 2012
- By Flora Mwakasala
- Imesomwa mara: 1109
WATU wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka ya kumtapeli mke wa Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja.
Washitakiwa hao Baraka Mkufunzi (28) na George Enos (45) wanakabiliwa na mashitaka 12 ya kujipatia Sh milioni 102.8 kwa njia ya udanganyifu na kujaribu kufanya usafirishaji haramu wa binadamu.
Walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Sakina Sinda, akisaidiana na Wakili Shadrack Kimaro mbele ya Hakimu Augustina Mmbando.
Ilidaiwa katika mashitaka ya kwanza kuwa kati ya Aprili mosi na Septemba 8, katika Wilaya ya Ilala Dar es Salaam, washitakiwa hao walitaka kusafirisha binadamu kinyume cha sheria.
Wakili Sinda alidai kuwa kati ya tarehe hizo, washitakiwa walijipatia Sh milioni tano kutoka kwa mke wa Kamishna Chagonja, Happyphania, kwa madai kuwa ni malipo ya maombi ya usajili wa mafunzo ya Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na ya Ofisi ya Usalama wa Taifa.
Wakili huyo alidai katika mashitaka mengine kuwa, kati ya tarehe hizo, washitakiwa walijipatia Sh milioni 22.3 kutoka kwa Issa Chikundi, Sh milioni 13.5 kutoka kwa Issa Rutemba, Sh milioni 3.7 kutoka kwa Daud Mgonja na Sh milioni 2.3 kutoka kwa Calota Ngowi.
Katika mashitaka mengine alidai washitakiwa walijipatia Sh milioni 11.4 kutoka kwa Emmanuel Chagonja, Sh milioni 1.4 kutoka kwa Dastan Mkwizu, Sh milioni 2.2 kutoka kwa Yudas Nkelane, milioni 1.4 kutoka kwa Ibrahim Hashim, Sh milioni 10.5 kutoka kwa Musa Hashim na Sh milioni 29.2 kutoka kwa Lauriana Joseph.
Alidai kuwa washitakiwa walijipatia fedha hizo kwa madai kuwa ni kwa ajili ya malipo ya maombi ya usajili wa mafunzo ya Polisi, Kitengo cha Takukuru na Usalama wa Taifa, jambo ambalo si kweli.
Washitakiwa walikana mashitaka na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kuwa na wadhamini wawili watakaotoa fedha taslimu Sh milioni 25 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kesi itatajwa Oktoba 2. Wakati huo huo, Mwandishi Wetu, Fadhil Abdallah anaripoti kutoka Kigoma kwamba askari Polisi wanne wa Kituo cha Mkugwa, Kibondo, wanashikiliwa kwa tuhuma za ujambazi.
Inadaiwa kuwa askari hao walimvamia na kumpora mfanyabiashara wa kijiji cha Kifura, Jenisa Minani Sh milioni mbili na kumjeruhi.
Taarifa zilizopatikana wilayani humo na baadaye kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Venance Mwamoto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, alisema hivi sasa askari hao wanashikiliwa Polisi, Kibondo.
Mwamoto alisema tukio hilo lilitokea usiku wa Septemba 18 katika kijiji cha Kifura, ambapo askari hao inadaiwa walimvamia mwanamke huyo alipokuwa akirejea nyumbani baada ya kufunga biashara zake.
Kwa mujibu wa habari hizo, askari hao walimvamia na kumjeruhi kwa mapanga na fimbo, jambo lililomsababishia maumivu makali.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wa kijiji hicho walivamia Kituo cha Polisi kijijini hapo wakiwa na silaha za jadi na kutaka kuchoma moto kituo hicho wakitaka kuwatoa askari hao na kuwaadhibu kwa kitendo cha kumvamia na kumdhuru mfanyabiashara huyo.
Hata hivyo, Mwamoto alisema amepata maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya kufanya uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikiana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa na maofisa wengine wa ngazi ya mkoa.
Pamoja na kutiwa mbaroni kwa tuhuma hizo, majina yao yamebaki kuwa siri kwa vyombo vya usalama kwa wanachoeleza kuwa majina hayo yatatangazwa itakapothibitika kwamba wamehusika na tukio hilo.


