23Mei2013

 

Sitta ang’ang’ana mafisadi watoswe

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Spika wa zamani wa Bunge, Samuel Sitta, ameibuka na kukitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuutumia uchaguzi wa mwaka huu kuzaliwa upya kwa kuwaondoa viongozi wanaojihusisha na rushwa na ufisadi vinginevyo kitakabiliwa na upinzani usio na sababu kutoka kwa vyama vidogo.

Pamoja na onyo hilo, Sitta alisema kamwe hataacha kukemea vitendo vya rushwa, dhuluma, ufisadi na ubabe vinavyofanywa na viongozi wa CCM na Serikali hata kama kwa kufanya hivyo ataambiwa kwamba anaipaka matope Serikali, huku akitamba kuwa tabia ya kusema ukweli imewafanya wapiga kura wake kumpachika jina la ‘Chuma cha Pua’.

Aliyasema hayo alipokuwa akiwahutubia wanafunzi, wazazi na walezi waliohudhuria mahafali ya 11 ya darasa la saba katika shule ya mchepuo wa Kiingereza ya Kwema iliyopo mjini hapa jana, katika hafla iliyohudhuriwa pia na Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM).

Katika hotuba yake hiyo pamoja na kuumwagia sifa uongozi wa shule hiyo, chini ya Mkurugenzi Mtendaji Pauline Mathayo na kuwapongeza pia wanafunzi 226 waliokabidhiwa vyeti jana katika shule hiyo inayofanya vizuri kutokana na mwaka jana kushika nafasi ya pili kitaifa na kutoa mwanafunzi namba 1, 3 na 5, kitaifa, alitumia muda mwingi kuwashambulia viongozi wa CCM na serikali wanaojihusisha na rushwa na ufisadi.

Alisema kutokana na kuwa na elimu, baadhi ya viongozi wa serikali wanaitumia vibaya elimu yao kwa kupanga mbinu za kupokea na kutoa rushwa kistadi na hivyo wananchi kutofahamu vitendo hivyo na kufanya rasilimali za Taifa kutoroshwa.

“Nimeambiwa na tatizo la kukosa umeme wa uhakika hapa Kahama wakati hapo mgodini (Buzwagi), kuna umeme wa kumwaga. Yaani Tanesco imetumia nguzo imara kuvuta umeme wa uhakika hadi mgodini, lakini bila kuwajali watu wa Kahama ambao wana matatizo makubwa ya umeme.

“Jambo hilo ni la kushangaza maana badala ya umeme kuwanufaisha wananchi unawanufaisha zaidi wageni. Mimi ndio maana huwa nasema halafu naambiwa naitia aibu wakati mimi ni sehemu ya Serikali.

Aibu ni aibu tu hata kama ni yako mwenyewe ni lazima isemwe. “Ni lazima viongozi wa serikali tujifunze kusema ukweli. Wapo viongozi wa serikali hawasemi ukweli hata kama wanaona wazi kwamba kuna tatizo. Mimi na Lembeli tutakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa umeme unaofika Kahama unakuwa ni wa uhakika,” alisema.

Waziri huyo ambaye alikuwa Spika wa Bunge la 9 linalotajwa kuwa Bunge lililokuwa na msisimko mkubwa, alisema wakati umefika sasa kwa Watanzania kutambulika kwa uadilifu na si kwa ufisadi, ubabe, dhuluma na rushwa.

“Wapo watu hadi sasa wanatuletea tabu katika nchi hii, bado wanaendeleza vitendo vya unyonyaji, dhuluma, rushwa, ufisadi, kuingia mikataba ya ovyo, kujenga miradi mibovu na hata barabara mbovu ambazo ndani ya miaka miwili zinabomoka na unashangaa viongozi wa serikali wanahusika. Haya ni mambo ya ovyo na yanaitia hasara na aibu nchi yetu.

“CCM kama chama tawala ni lazima ikemee tabia za wizi, dhuluma, ubabe, utoaji na upokeaji wa rushwa ili vitoweke. Tanzania haiwezi kuendelea kama hayo yataachwa yakaendelea.

Ni mwaka wa uchaguzi, CCM itumie fursa hii kuzaliwa upya. “Kuna maeneo tumetia aibu… rushwa, hakuna maamuzi badala yake waliobakia wanatamba ni wapaza sauti wa ufisadi. Zamani kule Uingereza na Ufaransa kulikuwa na watu wanaitwa wachekeshaji wa mfalme, kazi yao ilikuwa ni kumchekesha mfalme, kumuimbia na kumpiga fitna adui na walilipwa pesa na nguo kwa kazi hiyo.

“Ilifika siku mfalme alitembea uchi, lakini kwa vile kazi yao ni kumchekesha mfalme, walimsifia... mfalme umependeza…umevaa kanzu nzuri. “Hao ni viongozi wanaofikiria kwa matumbo na kuyafanya kuwa makubwa zaidi hadi kutaka kupasuka.

Ndio maana sasa CCM tunatukanwa hadi na tuvyama tudogo. Unashangaa mtu anakuwa kibaraka na anajivunia kuwa kibaraka. Viongozi kama hawa ni hatari, kwani wanatumia usiku na mchana kujipendekeza.

“WanaCCM ni lazima tushikamane ili kuwapata viongozi bora wanaofikiri kwa kichwa. Ukiwa mchekeshaji wa mfalme hata mkeo nyumbani anakucheka, anajua nyumbani tunapata pesa kutokana na uwakala wa ufisadi.Hawa watu washughulikiwe katika uchaguzi huu walichokifanya kinatosha,” alisema.

Kuhusu shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1996 ikiwa na wanafunzi 30 na sasa ikiwa na wanafunzi 1,840, ikiwa na mafanikio makubwa, Sitta alieleza kushangazwa na uwezo wa shule hiyo na kuahidi kutumia nafasi yake kama Waziri wa Afrika Mashariki kuzishawishi nchi zingine za jumuiya hiyo kuwasomesha hapo watoto wao.

“Hii ni aina ya shule ya kasi na viwango ninavyovitaka mimi. Shule inatoa mwanafunzi wa kwanza, wa tatu na wa nne kitaifa na halafu inakuwa ya pili kitaifa. Hili si jambo la mchezo hata kidogo. Naamini mwaka huu mwanafunzi wa kwanza, pili, tatu, nne… hadi saba huko watatoka hapa halafu kuanzia nane ndo tuwaachie wengine.”

Kabla, akimkaribisha Sitta, Lembeli alisema kizazi kinachohitimu masomo hivi sasa kinahitaji busara na hekima za kiongozi kama Sitta ambaye kwa muda mwingi amekuwa akipambana na vitendo vya rushwa na ufisadi hasa pale alipokuwa Spika wa Bunge.

Hafla hiyo pia ilitumika kuzindua Shule dada ya sekondari ya Kwema ambayo ilianza rasmi Januari mwaka huu, lakini kutokana na uwezo wake hivi sasa ina kidato cha pili kutokana na wazazi kuamua kuwapeleka watoto wao wa kidato cha pili shuleni hapo.