Tanesco Kilimanjaro watangaza hasara

SHIRIKA la Umeme (Tanesco) Mkoa wa Kilimanjaro, limepata hasara ya zaidi ya Sh milioni 258 kwa kipindi cha Septemba hadi Novemba mwaka huu, kutokana na wizi wa nyaya za shaba na transfoma.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanesco Mkoa wa Kilimanjaro, Maclean Mbonile, alisema hayo jana ofisini kwake wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alieleza kusikitishwa kwake na hujuma zinazofanywa na watu hao wanaoharibu miundombinu ya umeme. Mbonile alisema matukio ya wizi wa nyaya yametokea zaidi katika wilaya ya Mwanga.

Alisema yako matukio manane yaliripotiwa ya wizi wa nyaya za shaba. Wilaya ya Moshi, yako matukio ya uharibifu wa transfoma mbili na uchomaji nguzo za umeme.

Alisema nyaya za shaba zilizoibwa zina jumla ya urefu wa meta 4,145 na thamani ya zaidi ya Sh milioni 238, pamoja na transfoma mbili zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 20, ambazo ziliharibiwa kwa lengo la kuzitoa nyaya zake za ndani ambazo ni za shaba pia.

Mbonile alisema watu wanne wa wilayani Mwanga wanashikiliwa na Polisi kutokana na wizi huo wa nyaya hizo, ambapo kesi mbili zipo mahakamani zinazohusu watu waliojiunganishia umeme kinyemela.

Alisema kutokana na matukio hayo kuendelea, shirika hilo limetenga kati ya Sh 100,000 na milioni moja kwa wananchi watakaotoa taarifa za kweli, kuhusu wizi wa nyaya na trasfoma, viwanda vinavyotumia umeme wa wizi, watu waliojiunganishia umeme kinyemela kwa waliokatiwa.

Mbali na uharibifu huo meneja huyo alisema madeni katika taasisi za serikali kwa mwaka huu yamefikia Sh bilioni 4.3.